Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha linawashikilia watu sita kwa tuhuma za mauaji ya askari polisi, Roland Mollel, yaliyotokea usiku wa Aprili 15 katika eneo la Mlimani, Kata ya Muriet jijini Arusha.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo, tukio hilo lilitokea wakati askari huyo alipokuwa akifanya shughuli zake binafsi baada ya kazi.
Aidha amesema kabla ya tukio hilo kulizuka taharuki miongoni mwa wananchi kufuatia taarifa za kuwepo kwa watu waliodaiwa kuwa wezi katika eneo hilo.
Katika mkanganyiko huo, marehemu akiwa amepanda pikipiki pamoja na mtu mwingine anayedaiwa kuwa dereva wa bodaboda, walishambuliwa na kundi la watu waliokuwa wakiwafukuza kwa tuhuma hizo.
Polisi wamesema wanaendelea na msako wa kuwatafuta watuhumiwa wengine waliohusika na tukio hilo huku uchunguzi ukiendelea kukamilishwa.
Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi kuepuka kujichukulia sheria mkononi, huku likisisitiza kuwa vitendo hivyo ni kinyume cha sheria na vinaweza kusababisha madhara kwa watu wasio na hatia.






