Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, Camillus Wambura, amemzawadia kiasi cha shilingi milioni 5 mwanafunzi “Asiyeona” Winfrida Gilbert Wilson, kwa kutambua juhudi zake katika masomo na kuhitimu Kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Lugalo iliyopo mkoani Iringa na kuwa mfano wa mafanikio kupitia elimu licha ya changamoto alizonazo.
Akimkabidhi zawadi hiyo katika mahafali ya kuhitimu kidato cha sita katika Shule hiyo leo Aprili 16, 2026 kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Allan Bukumbi, amempongeza binti huyo na kumtakia heri katika mitihani yake, akieleza kuwa Jeshi la Polisi linaendelea kuthamini jitihada za vijana wanaopambana kufikia ndoto zao kupitia elimu.
Kwa upande wake Winfrida Wilson, amemshukuru Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania kwa zawadi hiyo, huku akisema fedha hizo zitamsaidia katika kuendelea na safari yake ya elimu na kumtia moyo wa kusonga mbele na kusoma kwa bidii zaidi.
Naye Mkaguzi wa Polisi (INSP) Ezron Magesa, ambaye amekuwa akimfadhili Winfrida kwa kiasi kikubwa, amempongeza kwa hatua kubwa aliyopiga na kueleza kuwa juhudi zake zimekuwa mfano wa kuigwa miongoni mwa jamii.
Kuhitimu kwa Winfrida ni mafanikio makubwa kwa Jeshi la Polisi Tanzania kupitia Kamisheni ya Polisi Jamii katika kuendelea kubaini, kuzuia na kutanzua uhalifu ndani ya jamii kupitia ushirikiano na uwezeshaji wa wananchi.






