Kamati za Mwenge wa Uhuru katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtama zimeendelea na vikao vya maandalizi kwa lengo la kuhakikisha mapokezi ya Mwenge huo yanafanyika kwa ufanisi na hadhi inayostahili.
Kikao cha hivi karibuni kimefanyika Aprili 16, 2026, kikilenga kukamilisha mikakati ya mwisho kabla ya ujio wa Mwenge wilayani humo.
Kikao hicho kimeongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtama, Anderson Msumbа, ambaye amesisitiza umuhimu wa ushirikiano na uwajibikaji kwa kila kamati ili kuhakikisha maandalizi yanakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
Amesema ni wajibu wa kila kamati kutekeleza majukumu yake kwa weledi na kwa wakati ili kuiwezesha wilaya hiyo kupokea Mwenge wa Uhuru kwa heshima inayostahili.
Aidha, amebainisha kuwa mawasiliano ya karibu kati ya kamati mbalimbali yatasaidia kuongeza ufanisi, kurahisisha utekelezaji wa majukumu na kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza.
Katika kikao hicho, wajumbe kutoka kamati mbalimbali waliwasilisha taarifa za utekelezaji wa majukumu yao, mafanikio yaliyopatikana pamoja na changamoto zilizopo, huku wakitoa mapendekezo ya namna ya kuzitatua kwa wakati.
Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kuwasili Wilaya ya Mtama Mei 1, 2026 ukitokea Wilaya ya Ruangwa, na utapokelewa rasmi katika Kambi ya Wachina Nyangao.
Kwa mujibu wa ratiba, mkesha wa Mwenge utafanyika katika Shule ya Msingi Kiwalala, huku maandalizi ya miundombinu na maeneo ya tukio hilo yakiendelea kuboreshwa ili kuhakikisha yanakuwa tayari kwa tukio hilo muhimu la kitaifa.






