Leo April 16 Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda, ameipongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini kwa ufanisi, hatua iliyowezesha upatikanaji wa huduma hiyo katika maeneo mengi ya mkoa huo na kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi, hususan sekta ya uvuvi.
Mhe. Mtanda alitoa pongezi hizo alipokutana na uongozi wa REA uliofika ofisini kwake kwa ajili ya mazungumzo, ikiwa ni sehemu ya ziara ya kutembelea miradi ya nishati pamoja na kushiriki mkutano wa washirika wa maendeleo ya nishati (RDPG).
Alieleza kuwa uchumi wa Mkoa wa Mwanza unategemea kwa kiasi kikubwa shughuli za uvuvi, na kwamba juhudi za REA kusambaza umeme pamoja na kutoa taa maalum zinazotumia nishati ya jua kwa ajili ya uvuvi wa dagaa zimekuwa msaada mkubwa, hasa katika uvuvi wa nyakati za usiku.
Aidha, Mhe. Mtanda alibainisha kuwa bado kuna visiwa na vitongoji ambavyo havijafikiwa na huduma ya umeme, lakini akasisitiza kuwa juhudi zinaendelea kuhakikisha maeneo hayo yanaunganishwa na nishati hiyo muhimu.
“Nawapongeza sana REA kwa kazi kubwa mnayoifanya. Hakuna ubaguzi katika utoaji wa huduma zenu kwani mnawahakikishia wananchi wote wanapata umeme, jambo linalochochea shughuli za uzalishaji.
Nawashukuru pia kwa kuwafikia wafugaji wetu, ikiwemo mfugaji tuliyemtembelea leo mwenye zaidi ya kuku 30,000,” alisema Mhe. Mtanda.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya REA, Balozi Meja Jenerali (Mstaafu) Jacob Kingu, aliwashukuru washirika wa maendeleo kwa mchango wao katika upatikanaji wa nishati vijijini.
Alisema ushirikiano huo umewezesha wananchi wengi kunufaika na huduma ya umeme pamoja na kuanzisha miradi mbalimbali ya kiuchumi.
Aliongeza kuwa REA itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha huduma ya umeme inawafikia wananchi wote, ikiwa ni sehemu ya kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.






