MATESO WANAYOPITIA WATOTO KATIKA MACHAFUKO YA SUDAN

Date:

Share post:

DARFUR, Sudan

“HALI ya watoto nchini Sudan inazidi kuwa mbaya kila baada ya saa moja.” Hiyo ni kauli ya Msemaji wa Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF), Eva Hinds.

Eva ameyasema hayo ukiwa ni mwaka wa tatu sasa tangu vita hivyo vilipoanza. Ripoti ya Umoja wa Mataifa (UN) inaeleza kuwa watu milioni 13 wamelazimika kuyakimbia makazi yao.

Ni vita kati ya pande hasimu mbili, Rapid Support Forces (RSF) na Sudanese Armed Forces (SAF), kila mmoja ukipigania kuiongoza Sudan.

Ripoti ya UNICEF inaeleza kuwa watoto zaidi ya 4,300 wameshauawa, huku Darfur na Kordofan yakitajwa kuwa ni maeneo yaliyohusika katika vifo vingi zaidi.

Ashan Abeywardena ambaye ni Meneja wa War Chird, Taasisi inayolinda usalama wa watoto walioko maeneo yenye vita, anasema:

“Kwa kipindi cha miaka mitatu ya vita, waathirika wakubwa wamekuwa ni watoto na wanawake. Habari za kila siku kuhusu watoto ni vifo na uharibifu tu.”

Kwa upande mwingine, ndege zisizo na rubani zinazotumiwa na wapiganaji wa pande zote mbili, kwa maana ya RSF na SAF, zimetajwa kuwa chanzo kikubwa cha mauaji na majeruhi.

Katika hilo, Eva wa UNICEF anasema: “Ndege zisizo na rubani zimekuwa zikijeruhi wasichana na wavulana wakiwa nyumbani, sokoni, barabarani, jirani na shule au hospitali. Hayo ni maeneo ambayo hayapaswi kushambuliwa.”

Kwa upande wake, Kiongozi wa Huduma za Kibinadamu wa UN, Tom Fletcher, amesema ndege hizo zimesababisha vifo vya raia takribani 700 kwa kipindi cha miezi mitatu ya hivi karibuni.

Taarifa za kiusalama zinaeleza kuwa RSF na SAF zimekuwa zikitumia ndege zisizo na rubani kushambulia miundombinu, ikiwamo ya usafiri, kwa lengo la kuzuiana.

Wakati huo huo, kwa mujibu wa mwandishi wa habari wa DW nchini Kenya, Andrew Wasike, mgogoro wa Sudan unaathiri kwa namna moja au nyingine nchi jirani ndani ya Ukanda wa Afrika Mashariki.

“Kwa Afrika Mashariki, athari za mgogoro huo haziwezi kuepukika,” amesema Wasike na kuzitaja athari hizo kuwa ni wakimbizi, kuharibika kwa njia za kibiashara na tishio la hali ya usalama.

Hata hivyo, Mkurgenzi wa masuala ya kibinadamu wa UN nchini Sudan, Denise Brown, haoni kama jumuhiya za kimataifa zimefanya vya kutosha katika kushughulikia kinachoendelea. Kwa mtazamo wake, ni kama dunia imetenga Sudan. “Swali langu ni je, dunia inasubiri nini?”

Lakini, walau kuna hatua imechukuliwa na kuibua matumaini kwa raia wa Sudan. Wiki iliyopita, Ujerumani ilikuwa mwenyeji wa Mkutano wa Kimataifa wa kuchangisha fedha za kuwasaidia waathirika wa vita nchini Sudan.

Kabla ya Mkutano kuanza mjini Berlin, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Johann Wadephul, alisema matarajio yao ni kukusanya Dola za Marekani bilioni moja, kama ilivyokuwa wakati wa Mkutano wa mwaka jana mjini London, Uingereza.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

spot_img

Related articles

GUARDIOLA AMPONZA KOCHA WA BURNLEY

LONDON, Uingereza KOCHA wa Burnley, Scott Parker, amekalia kuti kavu baada ya timu hiyo kufungwa bao 1-0 na Manchester...

BERNARDO AWEKA REKODI MPYA MAN CITY

MANCHESTER, Uingereza KATIKA ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Burnley, kiungo wa Manchester City, Bernardo Silva, ameweka rekodi ya...

MABOSI WAMTAKA BRUNO KUBAKI UNITED

MANCHESTER, Uingereza UONGOZI wa klabu ya Manchester United uko tayari kufanya lolote ili kumbakiza kiungo wake raia wa Ureno,...

CESC FABREGAS KOCHA MPYA CHELSEA?

LONDON, Uingereza KLABU ya Chelsea inaangalia uwezekano wa kumkabidhi benchi la ufundi kiungo wao wa zamani raia wa Hispania,...