KIONGOZI wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Leo XIV, yuko barani Afrika kwa ziara ya siku 10 katika mataifa ya Algeria, Angola, Cameroon na Guinea ya Ikweta.
Ukiacha Algeria yenye Waislam wengi, mataifa mengine matatu yanatajwa kuwa na idadi kubwa ya wafuasi wa Kanisa Katoliki.
Tofauti na mtangulizi wake, Papa Francis, Papa Leo hatokwenda Nigeria na DRC, ambazo zina idadi kubwa zaidi ya Wakatoliki barani Afrika.
KWANINI AFRIKA?
Papa Leo amechagua kulitembelea Bara hilo, kabla ya kwenda kwao Marekani au Amerika Kusini alikoishi kwa miaka mingi ya safari yake kwenye utumishi wa kiroho.
Mosi, wachambuzi wa siasa wanaamini Afrika imekuwa na ukaribu wa miaka mingi na Taasisi ya Kanisa Katoliki. Mathalan, uhusiano wake na Cameroon ulianza karne ya 19.
Kwa upande wa Angola, ilikuwa miongoni mwa nchi zilizopokea kwa mwitikio mkubwa ufuasi wa Kanisa Katoliki katika karne ya 15 na leo hii asilimia 40 ya raia wake ni wafuasi wa dhehebu hilo.
Pili, wachambuzi wanaamini changamoto lukuki za kijamii, kisiasa na kiuchumi zilizopo Afrika zimechagiza ziara ya Papa Leo.
Mfano; licha ya Rais Biya kung’ang’ania madaraka akiwa na umri mkubwa wa miaka 93, bado raia wengi ni masikini na hali ya usalama ni ya kutilia shaka katika maeneo mengi.
Ni kama ilivyo kwa Angola, ambapo vita kati ya wanajeshi wa Serikali na vikundi vya waasi imesabisha hali mbaya ya usalama, licha ya nchi hiyo kuwa na utajiri mkubwa wa mafuta.
Tatu, ziara ya Papa Leo inahusishwa na mkakati wa Kanisa Katoliki kuendelea kuimarisha ufuasi wake barani Afrika ili kukabiliana na nguvu ya dini na madhehebu mengine.
ANA KWA ANA NA MADIKTETA
Katika nchi zote anazotembelea, Papa amekuwa akikutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa kisiasa, pia akitembelea yatima na magereza.
Akiwa Cameroon, alikutana na Rais Paul Biya, ambaye ameiongoza nchi hiyo ya Afrika ya Kati kwa miaka mingi na sasa umri wake ni miaka 93.
Katika ziara yake ya mwisho, Papa Leo atakwenda Guinea ya Ikweta, ambako atakutana na Rais Teodoro Obiang Nguema Mbasogo.
Utawala wa Nguema Mbasogo unakosolewa vikali na jumuhiya za kimataifa, ikiwamo Marekani, ukitajwa kuwatesa wananchi, ikiwamo kuminya uhuru wa kujieleza kwa kuwafunga gerezani wakosoaji na wanasiasa wa upinzani.
Hata hivyo, kwa taratibu za Kanisa Katoliki, Papa katika ziara yake hapaswi kumgusa moja kwa moja kiongozi aliyeko madarakani, hata kama uongozi wake hauonekani kuwa msafi.
“Kuna njia nyingi za kuzungumza na mamlaka. (Papa) hupaswi kuwanyooshea kidole (viongozi walioko madarakani katika nchi uliyopo), bali kuna namna ya kuzungumza kidiplomasia na kutoa njia mbadala zinazoweza kusaidia,” anasema Askofu wa Dayosisi ya Sokoto ya Kaskazini-Magharibi mwa Nigeria.
NDOA ZA JINSIA MOJA
Mtangulizi wake, Papa Francis, alipotangaza Kanisa Katoliki kubariki ndoa za jinsia moja mwaka 2023, maaskofu wa nchi mbalimbali, zikiwamo Angola na Cameroon, waligomea wakisema ni kinyume cha mafundisho ya Biblia.
Kwa upande wa Papa Leo, amekuwa na kigugumizi juu ya hilo – hajawahi kubariki wala kuonesha kutokukubaliana na utamaduni huo unaopingwa na wengi.
UJUMBE WAKE
Msisitizo mkubwa wa Papa Leo katika ziara yake barani Afrika ni umuhimu wa kutunza amani, akilaani machafuko yanayoendelea duniani.
Kwa upande wa Afrika, amewataka viongozi walioko madarakani kushirikiana na wananchi katika kutunza amani, umoja na mshikamano.
Akieleza hilo nchini Cameroon, Papa Leo alinukuliwa akilaani vitendo vya rushwa, akisema vimekuwa chanzo cha kukosekana kwa usawa katika jamii na Taifa kwa ujumla.
Katika hotuba zake, ameeleza umuhimu anaouona kwa Afrika kuwa kitu moja, badala ya kujigawa kwa misingi ya tofauti ya rangi, dini, mipaka ya kisiasa, na viwango vya kiuchumi.






