TAIPEI, Taiwan
RAIS wa Taiwan, Lai Ching-te, ameahirisha ziara yake nchini Eswatini, huku akiitaja China kuwa ndiyo chanzo cha uamuzi wake huo.
Mataifa hayo yamekuwa kwenye mvutano wa miaka mingi, huku kukiwapo kwa tishio la China kuivamia kijeshi Taiwan.
Ching-te amesema mamlaka za China zimesababisha kukwama kwa safari yake kutokana na kuweka shinikizo kwa baadhi ya nchi kuzuia ndege yake kutumia anga zake.
Sshelisheli, Mauritius na Madagascar zimeripotiwa kuinyima kibali ndege ya kiongozi huyo kupita kwenye mipaka yake ya anga.
Hatua hiyo imetokana na China kuzipa vitishio vya kuziwekewa vikwazo vya kiuchumi endapo zingeruhusu ndege ya Rais Ching-te kutumia anga zake.
Aidha, China imekanusha taarifa hizo, ikisema haijaweka vitisho vya aina hiyo, licha ya kupongeza hatua iliyochukuliwa na mataifa hayo ya Afrika.






