BERLIN, Ujerumani
RAIS wa Brazil, Luiz Inacio Lula da Silva, amesema Donald Trump hana mamlaka ya kumzuia Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini kushiriki Mkutano wa G20.
Akizungumza mjini Hannover, Ujerumani jana Aprili 20, 2026, Da Silva amemtaka Rais Ramaphosa kupuuzia kauli za Trump, na badala yake kuhudhuria Mkutano huo.
“Nimemwambia Ramaphosa kwamba anapaswa kuhudhuria Mkutano wa G20. Anapaswa kuwepo. Hawezi kukosekana eti kwa sababu Trump ameamua,” amesema.
Inafahamika kuwa uhusiano wa Afrika Kusini na uongozi wa Rais Trump umezorota kwa miaka ya hivi karibuni.
Kutokana na madai yake kuwa Serikali ya Afrika Kusini imekuwa ikisimamia mauaji ya watu weupe nchini humo, Trump amechukua hatua kadhaa dhidi ya uongozi wa Rais Ramaphosa.
Mbali ya kuzuia misaada ya kifedha, pia ametoa nafasi kwa watu weupe wa Afrika Kusini kwenda kuishi Marekani endapo wanahisi kudhulumiwa haki zao katika Taifa hilo la Afrika.






