LONDON, Uingereza
WOLVES imeiaga Ligi Kuu ya England (EPL) baada ya kushuka daraja. Timu hiyo inarejea Championship ikiwa ni miaka nane tangu ilipotoka huko.
Novemba, 2025, mabosi wa klabu hiyo walimuajiri kocha Rob Edwards ili kuokoa jahazi lakini ameshinda mechi tatu pekee kati ya 22 za Ligi alizokaa kwenye benchi.
MAKOSA YA USAJILI
Baada ya kuwauza mastaa Raul Jimenez, Diogo Jota, Ruben Neves, Matheus Cunha na Rayan Ait-Nouri, Nelson Semedo na Pablo Sarabia kwa nyakati tofauti, Wolves haikuweza kuziba mapengo yao.
Kati ya wengi waliosajiliwa majira ya kiangazi, 2024, hakuna mchezaji wa kikosi cha kwanza. Emmanuel Agbadou, Nasser Djiga na Marshall Munetsi walisajiliwa Januari, 2025 ili kuipa nguvu timu hiyo.
Matokeo yake, Agbadou alifeli na kuuzwa Besiktas, wakati Djiga na Munetsi walitolewa kwa mkopo.
Wakati wa usajili wa kiangazi, 2025, alisajiliwa winga Jhon Arias akitokea Fluminense lakini alichemsha na kuuzwa Palmeiras. Fer Lopez naye alisajiliwa kipindi hicho, kabla ya kurudishwa Celta Vigo kwa mkopo.
Nyota wengine waliosajiliwa lakini hawana mchango mkubwa kikosini ni David Moller Wolfe, Tolu Arokodare na Jackson Tchatchoua, ambao wakigharimu Pauni milioni 45.
KUFUKUZA MAKOCHA
Wolves imenolewa na makocha saba tofauti tangu Nuno Espirito Santo alipoondoka mwaka 2021, akiwamo Steve Davis aliyedumu katika mechi nane tu mwaka 2022.
Nuno raia wa Ureno, ndiye kocha aliyeipandisha Daraja mwaka 2018, akiiwezesha pia kumaliza katika nafasi ya saba mara mbili mfululizo Ligi Kuu ya England, kufika robo fainali ya Ligi ya Europa na nusu fainali ya FA.
Aliondoka mwaka 2021 akiiacha timu hiyo ikiwa imemaliza msimu katika nafasi ya 13 kwenye msimamo wa Ligi.






