RIPOTA PANORAMA – 0711 46 49 84
JESHI la Polisi limewaruhusu wanafunzi saba wanaosoma kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya St. Mary’s waliokamatwa wakivuta dawa za kulevya aina bangi kufanya mitihani ya kumaliza kidato cha nne.
Akizungumza leo na Tanzania PANORAMA Blog, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni (RPC), Kamishna Msaidizi, Ramadhani Kingai amesema polisi imewaruhusu wanafunzi hao kufanya mitihani ya kumaliza elimu ya sekondari kwa sababu za kiutu na watakapomaliza hatua za kisheria dhidi ya tuhuma zao zitachukuliwa.
RPC Kingai amesema atatoa taarifa ya hatua zitakazochukuliwa na polisi Jumatatu, Oktoba 7, 2020 ambapo watakuwa wamekamilisha uchunguzi ukiwemo wa kutoweka kwa mwanafunzi aliyekuwa akisoma kidato cha tatu katika shule hiyo, Labna Salim Said.
Vijana hao saba ambao majina yao hayajatajwa walikamatwa wakivuta na wakiwa na misokoto ya bangi ndani ya nyumba ya Kamishna wa Jeshi la Magereza wakati wa msako wa Labna na baada ya nyumba hiyo kupekuliwa ilingulika kuwa na shamba la bangi ndani ya ua unaoizunguka.
RPC Kingai alikataa kulitaja jina la Kamishna huyo na mahali ilipo ambamo walikutwa vijana hao wakiwa na misokoto ya bangi pamoja na shamba la bangi.
Katika hatua nyingine, RPC Kingai alisema hadi sasa polisi haijafanikiwa kumpata mwanafunzi Labna lakini juhudi za kumtafuta zinaendelea.
Mwanafunzi msichana Labna wa Shule ya Sekondari ya Bweni ya St. Mary’s iliyoko Mbezi Makonde alitoweka shuleni tangu Oktoba 4, 2020 na kutokomea kusikojulikana na hadi sasa hajapatikana.
Labna alitoweka akiwa chini ya uangalizi wa shule ya St, Mary’s na taarifa za kutoweka kwake zilitolewa Oktoba 8, 2020 na matron wake, Sarah Murra aliyempigia simu mama mzazi wa Labna akiulizia kama ameishafika nyumbani.
Uongozi wa Shule ya Sekondari ya St. Mary’s haukutoa taarifa polisi kuhusu kutoweka kwa mwanafunzi huyo na badala yake wazazi ndiyo walioripoti tukio la mtoto wao kupotea akiwa shuleni.