PORTO-NOVO, Benin
NI rasmi sasa aliyekuwa Waziri wa Fedha wa Benin, Romuald Wadagni, ndiye Rais mpya wa Taifa hilo baada ya ushindi wa asilimia 94 ya kura katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Jumapili ya Aprili 12, 2026.
Hata kabla ya matokeo ya mwisho kutangazwa, mgombea wa upinzani katika kiti cha urais, Paul Hounkpe, alishakubali kushindwa, akisisitiza nia yake ya kutaka Taifa hilo lisigawanyike.
Wadagni anachukua nafasi aliyekuwa bosi wake katika awamu iliyopita, Patrice Talon, ambaye hata hivyo anakosolewa kwa kuvibana mbavu vyama vya upinzani.
Hilo lilithibitika baada ya Chama kikuu cha upinzani, Democrats, kushindwa kusimamisha mgombea katika nafasi ya urais.
Hata hivyo, changamoto kubwa inayomkabili Rais mpya, ambaye atakuwa madarakani hadi mwaka 2033, ni pamoja na kiwango kikubwa cha umasikini kwa raia na rushwa katika taasisi za umma.
Imeandaliwa na Hassan Mwasha






