Washington DC, Marekani
Huu si mzozo wa makombora wala si vita ya silaha nzito, bali ni vita ya maneno iliyozua gumzo duniani kati ya Rais wa Marekani, Donald Trump, na Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Leo XIV.
Mvutano huo ulianza baada ya Rais Trump kutoa kauli kali akimtaka Papa Leo aache kuingilia masuala ya kisiasa, akidai hana uelewa wa kutosha kuhusu siasa za kimataifa na badala yake ajikite kwenye majukumu ya kidini.
Lakini haikuishia hapo.
Trump alienda mbali zaidi kwa kumshambulia Papa kwa maneno mazito, akimtaja kuwa “dhaifu na muhalifu,” huku akidai kuwa kuchaguliwa kwake kunalenga kuishughulikia Serikali ya Marekani iliyopo madarakani. Kauli hiyo imechukuliwa na wengi kama shambulio la moja kwa moja dhidi ya mamlaka ya Vatican na ushawishi wa Kanisa Katoliki katika masuala ya kimataifa.
Chanzo cha hasira ya Trump kinaelezwa kuwa ni kauli ya awali ya Papa Leo XIV, ambaye alionyesha wazi kuwa haungi mkono vitisho vya Marekani dhidi ya Iran. Vilevile, Papa alikosoa namna utawala wa Trump unavyoshughulikia suala la wahamiaji haramu nchini humo.
Baada ya Trump kumtaka Papa ajitenge na siasa, Papa Leo XIV naye hakusita kujibu. Kwa msimamo thabiti, alisema hatishwi na utawala wa Trump na ataendelea kukosoa hatua yoyote anayoona inaleta madhara kwa amani ya dunia, hususan mashambulizi dhidi ya Iran.
“Sihofii utawala wa Trump, wala kupaza sauti kusambaza neno la Mungu… Sitaki mjadala naye. Watu wengi sana wanapitia mateso duniani. Wengi wasio na hatia wanauawa. Nafikiri mtu anapaswa kusimama na kusema…,” alisema Papa Leo XIV.
Kauli hiyo imeongeza moto kwenye mjadala ambao sasa umegeuka kuwa gumzo la kimataifa, hasa ikizingatiwa kuwa Trump na Makamu wake, JD Vance, ni sehemu ya Wakatoliki zaidi ya milioni 70 waliopo Marekani, idadi inayokadiriwa kufikia asilimia 20 ya raia wote wa taifa hilo.
Mvutano huu umeibua maswali mazito: je, Rais wa Marekani anaweza kushambulia hadharani kiongozi wa dini mwenye ushawishi mkubwa duniani bila athari za kisiasa na kidiplomasia?
Wengi wanaamini tayari Trump amevuka mpaka.
Baadhi ya waumini na wachambuzi wa masuala ya Kanisa wanasema hatua hiyo ni nadra kutokea katika historia ya uongozi wa Marekani. Massimo Faggioli, mmoja wa waumini wa Kanisa Katoliki, amesema kauli za Trump zinaonesha kiwango kipya cha uhasama dhidi ya Vatican.
“Hata madikteta Hitler na Mussolini hawakuwahi kumshambulia Papa hadharani,” anasema Faggioli.
Wengine wanaona msimamo wa Papa Leo XIV kuhusu Iran si jambo la ajabu, bali ni sehemu ya msimamo wa muda mrefu wa Kanisa Katoliki kuhusu kuhimiza amani na kukemea vita.
“Kwa karne tano zilizopita, Kanisa limekuwa na miradi ya kuhimiza mshikamano wa kimataifa,” anasema Profesa William Barbieri wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki.
Kwa upande mwingine, wachambuzi wanaona Papa Leo XIV huenda anafuata nyayo za mtangulizi wake, Papa Francis, ambaye aliwahi kuingia kwenye mvutano mkubwa na Trump wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Marekani mwaka 2016.
Papa Francis (sasa marehemu) aliwahi kusema Trump “si Mkristo,” kauli aliyotoa wakati akikosoa matamshi aliyoyaita ya kibaguzi dhidi ya wahamiaji haramu. Kauli hiyo ilizua taharuki kubwa na kuacha doa kwenye uhusiano wa Trump na Kanisa Katoliki kwa miaka kadhaa.
Hata hivyo, tofauti na Papa Francis ambaye mara nyingi alizungumza kwa tahadhari ya kidiplomasia, Papa Leo XIV anaonekana kuchukua msimamo wa wazi na wa moja kwa moja zaidi—jambo linaloonekana kumkera Trump.
Katika hatua nyingine iliyowahi kuibua mjadala, utawala wa Trump uliripotiwa kulionya Kanisa Katoliki, ukidai linapaswa kujiweka mbali na mipango ya jeshi la Marekani. Tukio hilo linaonesha kuwa uhusiano kati ya Trump na Kanisa Katoliki haujawahi kuwa wa amani ya kudumu.
Kadri siku zinavyosonga, mzozo huu unaendelea kuwa zaidi ya mabishano ya maneno. Ni ishara ya mapambano ya ushawishi kati ya mamlaka ya kisiasa ya Marekani na mamlaka ya kiroho ya Vatican—mapambano yanayoweza kuathiri si tu taswira ya Trump ndani ya jamii ya Wakatoliki, bali pia nafasi ya Vatican katika kusimamia masuala ya amani na haki duniani.
Na wakati dunia ikitazama, swali kubwa linabaki: je, huu ni mwanzo wa uhasama mpya kati ya Marekani na Vatican, au ni kelele za kisiasa zitakazopoa kadri muda unavyopita?






