London, Uingereza
Klabu ya Chelsea imeendelea kuonyesha nia ya dhati ya kumsajili kiungo wa pembeni wa FC Porto, William Gomes, huku taarifa zikieleza kuwa maskauti wa Blues tayari wamewasili nchini Ureno kwa ajili ya kufuatilia kwa karibu maendeleo ya nyota huyo wa kimataifa wa Brazil.
Gomes amekuwa gumzo kubwa msimu huu kutokana na kiwango chake bora, akionekana kuwa miongoni mwa wachezaji wanaowaka zaidi kwenye kikosi cha Porto. Winga huyo amefunga mabao 13 na kutoa pasi mbili za mabao (‘asisti’) katika jumla ya michezo 40 aliyocheza kwenye mashindano mbalimbali.
Chelsea inaonekana kuvutiwa na uwezo wake wa kushambulia, kasi pamoja na ubunifu wake uwanjani, sifa ambazo zinaendelea kumfanya aonekane kama mchezaji mwenye uwezo wa kuipa nguvu safu ya mbele ya kikosi hicho cha Stamford Bridge.
Porto ilinasa saini ya Gomes mwanzoni mwa mwaka 2025 baada ya kuvutia kwa kiwango cha juu alipokuwa akiitumikia Sao Paulo ya Brazil. Tangu kujiunga na timu hiyo ya Ureno, ameendelea kupanda thamani na kuonyesha kuwa ni mali muhimu ndani ya kikosi.
Katika mkataba wake wa sasa, Sao Paulo ina kipengele kinachowapa fursa ya kuvuna asilimia 20 ya fedha zitakazopatikana endapo Porto itamuuza kwa klabu nyingine, jambo linalomaanisha kuwa dili lolote litakalokamilika litawanufaisha pia mabingwa hao wa zamani wa Brazil.
Hadi sasa Chelsea haijatoa ofa rasmi, lakini uwepo wa maskauti wao nchini Ureno unaashiria wazi kuwa huenda dili hilo likawa moja ya usajili mkubwa unaoweza kushika kasi kwenye dirisha lijalo la usajili.
Imeandaliwa na Hassan Mwasha






