Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ametembelea na kukagua maendeleo ya mradi wa Mji wa AFCON Fumba uliopo Mkoa wa Mjini Magharibi.
Ziara hiyo imefanyika leo Aprili 14, 2026, ambapo Rais Mwinyi aliambatana na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dkt. Riziki Pembe Juma, pamoja na wadau mbalimbali wa mradi huo.
Katika ukaguzi huo, Rais Mwinyi alipata fursa ya kutembelea na kujionea hatua mbalimbali za ujenzi wa uwanja wa kisasa wa AFCON unaojengwa na kampuni ya ORKUN Group ya Uturuki. Uwanja huo unatarajiwa kutumika katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2027, ambayo itaandaliwa kwa ushirikiano wa nchi za Afrika Mashariki za Kenya, Uganda na Tanzania.
Aidha, Rais Mwinyi alikagua pia miundombinu mingine inayotarajiwa kuzunguka uwanja huo, ikiwemo hospitali, barabara, migahawa na maduka makubwa (mall). Miradi hiyo inalenga kuboresha huduma za kijamii na kukuza maendeleo ya mji huo wa kisasa.









