ACCRA, Ghana
ALIYEWAHI kuwa kocha msaidizi wa Manchester United wakati ule wa Alex Ferguson, Carlos Queiroz, amekabidhiwa mikoba ya kuinoa timu ya Taifa ya Ghana ‘Black Stars’ inayojiandaa na fainali za Kombe la Dunia za mwaka huu.
Queiroz (73), anachukua mikoba ya Otto Addo, ambaye aliachia benchi Machi 31, 2026 baada ya Black Stars kupoteza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Austria na Ujerumani.
Kocha huyo anaikuta timu hiyo ikiwa hoi kwani pia ilishindwa kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika zilizopita (AFCON 2025).
Anatua kikosini akiwa na uzoefu mkubwa wa kuzinoa timu za taifa, zikiwamo Afrika Kusini, Ureno, Iran, Colombia na Misri.
Katika fainali za Kombe la Dunia zitakazoanza Juni, 2026, Ghana imepangwa Kundi L na itacheza mechi yake ya kwanza dhidi ya Panama (Juni 17).
Imeandaliwa na Hassan Mwacha






