Sunday, June 29, 2025
spot_img

MWANZA WAMUAGA HAYATI RAIS DK. MAGUFULI KISHUJAA

 

Akinana mkoani Mwanza wakipunga mkono wa buruani kwenye jeneza la Hayati Rais Dk. John Pombe Magufuli (halipo Pichani)

NA MWANDISHI WA PANORAMA

WAKAZI wa Mkoa wa Mwanza na viunga vyake wamemuaga kishujaa, Hayati Rais Dk. John Pombe Magufuli aliyefariki dunia Machi 17, 2021 katika Hospitali ya Mzena iliyopo Mkoa wa Dar es Salaam kutokana na maradhi ya moyo.

Mwili ya Hayati Rais Dk. Magufuli uliwasili mkoani Mwanza majira ya asubuhi ukitokea Zanzibar na kupokewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla,   Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela, viongozi wa chama na serikali pamoja na umati mkubwa wa wananchi wa Mkoa wa Mwanza na mikoa ya jirani.

Kutoka Uwanja wa Ndege wa Mwanza, mwili wa Hayati Rais Dk. Magufuli uliokuwa katika gari maalumu la kijeshi, ulipitishwa katika vitongoji vilivyokuwa na umati mkubwa wa watu waliojitokeza kumpa mkono wa buriani vya Ilemela, Pasiansi, Nyamanoto, Selemani Nassoro, eneo ambalo ana nyumba yake aliyokuwa akiishi wakati akifanya kazi mkoani Mwanza, Ghana, Furahisha hadi Uwanja wa CCM Kirumba ambako viongozi  na wananchi walipata fursa ya kuaga na kutoa heshima za mwisho zilizoongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Mazishi Kitaifa.

Msafara wenye mwili wa Hayati Rais Dk. John Magufuli ukipita eneo la Furahisha huku umati wa wananchi wa Mkoa wa Mwanza uliojitokeza kumuaga ukipunga mkono wa burunani

 

Kabla kuaga na kutoa heshima za mwisho, Waziri Mkuu Majaliwa ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mazishi kitaifa, alitoa salamu za Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na serikali kwa wananchi wa Mwanza kwa kueleza kuwa Hayati Rais Dk. Magufuli alikuwa kiongozi mahiri na ameacha alama taifa zima ndiyo maana analiliwa na wananchi nchi nzima, hadi vijijini.

“Mpendwa wetu, kaka yetu, kiongozi wetu Dk. John Pombe Magufuli alikuwa kiongozi shupavu aliyeliongoza taifa hili kwa umahiri mkubwa na Mwanza ni mahali pa kihistoria kwa kiongozi wetu, ameishi hapa, amefanya kazi hapa na katika utumishi wake amefanya mambo makubwa ambayo yameweka alama kwenye mikoa hii ya Kanda ya Ziwa,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Alisema Rais Samia anawapa pole wananchi wa Kanda ya Ziwa na anawasihi waendelee kuwa watulivu, kushikamana, kupendana kama ilivyo ada ya Watanzania katika kipindi hiki kigumu.

Waziri Mkuu Majaliwa alitoa rai kwa Watanzania wote, kila mmoja kwa imani ya dini yake na dhehebu lake aendelee kumuomba Mwenyezi Mungu aiweke roho ya Hayati Rais Dk. Magufuli pema peponi.

Wananchi wa Mkoa wa Mwanza wakikimbia sambamba na msafara wenye mwili wa Hayati Rais Dk. John Magufuli   


 

 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya