LAGOS, Nigeria
WAHENGA walisema maisha ni safari yenye milima na mabonde. Kwamba katika kuishi kwako, si nyakati zote zitakuwa za furaha, hivyo unapaswa kujiandaa na changamoto zinazoweza kujitokeza.
Changamoto ambazo, bila kujali ukubwa wake, hazipaswi kukuvunja na kufanya ukate tamaa, bali kukuimarisha katika kuzifikia ndoto ulizonazo.
Ndicho walichokifanya watu maarufu wengi. Changamoto hazikuwarudisha nyuma, bali walizitumia kama chombo cha usafiri kuzifikia ndoto zao.
PATORANKING
Staa wa muziki wa Afrobeats. Patoranking ni mmoja ya wanamuziki wenye majina na utajiri mkubwa kwa sasa nchini Nigeria.
Kabla ya kuingia kwenye sanaa na kumlipa, nyota huyo alikuwa akijihusisha na biashara ya kuuza dawa za panya huko mitaani.
Patoranking alifichua hilo mwaka 2024, aliposema: “Nikiwaambia kuwa niliowahi kuuza dawa za panya mtaamini?”
BANKY W
Nyota wa muziki nchini Nigeria, ambaye kabla ya kuingia na ‘kutoboa’ kupitia muziki, aliwahi kufanya kazi nyingi za kipato cha chini ili kumudu maisha.
Akiwa Marekani kwa masomo, Banky W, ambaye jina lake halisi ni Olubankole Wellington, aliwahi kujiingiza katika biashara ya kuuza visu majumbani.
Wakati mwingine, pia aliweza kufanya kazi ya kuuza ‘baga’ katika Mgahawa wa McDonald ili tu maisha yaende.
P-SQUARE
Paul na Peter Okoye ni mapacha waliowahi kutikisa soko la muziki barani Afrika kupitia Kundi lao la P-Square. Kabla ya ustaa, maisha yao hayakuwa rahisi.
Paul alikuwa fundi wa umeme, wakati Peter alijikita katika utengenezaji wa feni. Mwaka 2014, Peter alisema: “Nilikuwa fundi wa vifaa vya umeme, zikiwamo feni.
TIMAYA
Huyo naye ni mwamuziki maarufu wa Afrobeat. Kabla ya mafanikio makubwa aliyonayo sasa, Timaya alikuwa mmoja ya vijana waliokuwa wakiuza ndizi mitaani.
Alifichua hilo mwaka 2021, aliposema: “Niliwahi kuuza ndizi na sasa ni tajiri. Niliteseka sana lakini sasa ni tajiri. Asante Mungu.”
MERCY JOHNSON
Bibiye mwenye jina kubwa kwenye kiwanda cha filamu za Nigeria (Hollywood). Kabla ya ustaa alionao, Mercy aliwahi kuwa mfanyakazi wa ndani.
Katika moja ya mahojiano yake, alisema: “Unajua kuwa niliwahi kuwa mfanyakazi wa ndani na kufanya kazi zingine za kipato kidogo ili tu kujikimu?”
Pia, Mercy alifichua alivyowahi kuacha shule kutokana na muda mwingi aliokuwa akitumia kutafuta maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.






