NINI CHANZO CHA ‘BIFU’ ZITO LA MAPACHA WA P-SQUARE?

Date:

Share post:

LAGOS, Nigeria

MAMBO yamezidi kuwa mabaya kwa mapacha waliowahi kutikisa soko la muziki barani Afrika kupitia Kundi la P-Square, Peter na Paul Okoye.

Okoye ametangaza rasmi kubadili tarehe yake ya kuzaliwa ili asiwe anachangia ‘birthday’ na ndugu yake, Paul.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X, amesema kwa sasa birthday yake haitakuwa Novemba 18 kama zamani.

“Natangaza rasmi. Novemba 18 siyo tena tarehe yangu ya kuzaliwa. Ifahamike kuwa sitopokea meseji za pongezi wala zawadi katika siku hiyo,” amesema na kudokeza kuwa birthday yake itakuwa Novemba 30.

Hatua hiyo ni mwendelezo wa uadui mkubwa uliopo kati ya mapacha hao. Mwaka 2025, Peter alitangaza kuwa kwa sasa hataki ukaribu na familia yao yote.

Je, zipi sababu za mapacha hao kuwa ‘chui na paka’? Makala haya yanachambua, yakianzia historia ya Kundi la P-Square.

Peter na Paul walianzisha P-Square mwaka 2003. Ni kundi lililopata umaarufu mkubwa si tu Nigeria, bali pia ndani na nje ya Afrika.

Miaka miwili baadaye, waliingiza sokoni albamu yao ya kwanza, ‘Get Squared’, iliyokuwa na ngoma kali, ikiwamo ‘Bizzy Body’.

Mwaka 2015, wakiwa tayari ni wasanii wakubwa na wenye mafanikio, ikiwamo albamu yao kali ya ‘The Invasion’, ilianza kusikika minong’ono juu ya uhusiano wao kutikisika.

Nyuma ya pazia, zilitajwa sababu mbalimbali zilizosababisha mgogoro. Miongoni mwanzo ni masuala ya fedha.

Mwaka 2017, jipu lilipasuka rasmi baada ya wawili hao kutangaza kuvunjika kwa Kundi la P-Square. Peter ndiye aliyetangaza kujitoa kwa madai ya kutokuwapo na maelewano kati yake, Paul na uongozi (kaka yao aitwaye Jude).

Wakati mambo yakiwa hivyo, ilivuja video ikiwaonesha Paul na Peter wakikaribia kurushiana makonde mbele ya mwanasheria.

Baadaye, waliuza nyumba waliyokuwa wakimiliki pamoja kama P-Square na kila mmoja akapata mgawo wake na kuendelea na maisha.

Peter alianza kujiita ‘Mr. P’, wakati Paul ambaye inaelezwa kuwa bado anaungwa mkono na kaka yao, Jude, aliona ajiite ‘Rudeboy’.

Mwaka 2021, walionekana mara kadhaa wakifanya shoo pamoja, kabla ya kurejesha Kundi lao la P-Square na kuachia ngoma kadhaa, zikiwamo ‘Jaiye’ na ‘Find Somebody’.

Hata hivyo, mwaka 2024 wawili hao walitemana tena. Kwa mujibu wa Paul, Peter alimtumia meseji akimwambia havutiwi kuendelea kufanya naye kazi.

Paul hakuishia hapo. Alisema Peter ‘alimchoma’ yeye na kaka yao, Jude, kwa Taasisi ya Uhalifu wa Kiuchumi (EFCC) kwa madai ya utakatishaji fedha.

Kama itakumbukwa, Paul aliitwa na kuhojiwa na EFCC, kabla ya kuachiwa baada ya kukutwa hana hatia.

Mbali ya masuala ya fedha, zipo sababu zingine zinazotajwa kuchangia ‘damu mbaya’ kati ya Peter na Paul.

Peter amewahi kusema alichukuliwa kama mfanyakazi katika Kundi na si sehemu ya wamiliki. Kutokana na hilo, aliomba kaka yao, Jude, asiendelee kuwa meneja, jambo ambalo hakusikilizwa.

Pia, kuna suala la familia. Zipo taarifa kuwa Peter hakuwa akifurahia namna mkewe, Lola Omotayo, alivyokuwa akipuuzwa na kaka yao, Jude, na ndugu wengine wa familia yake.

Vilevile, kitendo cha mashabiki kujenga mijadala ya nani mkali kati ya Paul na Peter kilitengeneza wivu na chuki kati ya wawili hao, hivyo kuliangusha Kundi hilo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

spot_img

Related articles

USIYOYAJUA KUHUSU ZIARA YA PAPA LEO BARANI AFRIKA

KIONGOZI wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Leo XIV, yuko barani Afrika kwa ziara ya siku 10 katika mataifa...

MATESO WANAYOPITIA WATOTO KATIKA MACHAFUKO YA SUDAN

DARFUR, Sudan "HALI ya watoto nchini Sudan inazidi kuwa mbaya kila baada ya saa moja." Hiyo ni kauli ya...

IRAN: TUKO TAYARI KWA VITA MAZUNGUMZO YAKISHINDIKANA

TEHRAN, IranSPIKA wa Bunge la Iran, Mohammad Bagher Ghalibaf, amesema nchi yake itakuwa tayari kwa mbinu mpya za...

RAIS WA BRAZIL AMVAA TRUMP, AITAKA AFRIKA KUSINI KUMPUUZA

BERLIN, Ujerumani RAIS wa Brazil, Luiz Inacio Lula da Silva, amesema Donald Trump hana mamlaka ya kumzuia Cyril Ramaphosa...