Serikali, kupitia Wizara ya Afya, imeendesha zoezi la kupima utayari wa wataalamu wa afya na sekta mbalimbali katika kukabiliana na dharura za afya ya umma, ikiwemo mlipuko wa ugonjwa wa Ebola, mkoani Kigoma.

Lengo la zoezi hilo ni kutathmini uwezo wa sekta zinazohusika moja kwa moja na udhibiti wa dharura za afya, pamoja na kukagua mifumo ya mawasiliano, uratibu na utoaji wa huduma endapo kutatokea mlipuko wa ugonjwa huo.

Mwakilishi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mwanaisha Mrisho, amesema zoezi hilo linasaidia kubaini kiwango cha utayari wa Mkoa wa Kigoma katika kukabiliana na dharura za afya ya umma, ikiwemo Ebola.

Akifungua mafunzo hayo yaliyofanyika mjini Kigoma, Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Zabibu Mkamba, amesema mkoa huo una wilaya sita zinazopakana na nchi jirani, hali inayoweka wajibu mkubwa kwa wataalamu wa afya kuhakikisha maeneo hayo yanakuwa salama dhidi ya magonjwa ya mlipuko.

Ameongeza kuwa endapo ugonjwa huo utaingia nchini, maandalizi hayo yatawezesha mamlaka husika kuudhibiti mapema na kuzuia usambazaji wake kwa jamii.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here