Kijiji cha Sango, kilichopo Kata ya Kimochi, Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, imezinduliwa rasmi katika mwendelezo wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2026.
Uzinduzi huo unalenga kuimarisha utoaji wa huduma za kiutawala pamoja na kurahisisha upokeaji na utatuzi wa kero za wananchi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Wazo Michael Mwang’onda, alisema mradi huo umekamilika kwa kuzingatia viwango vya kitaalamu baada ya kufanyiwa ukaguzi na kuthibitishwa kuwa unakidhi ubora unaotakiwa.
“Ukaguzi uliofanyika umebaini kuwa jengo hili limejengwa kwa ubora unaokubalika na linakidhi viwango vinavyotakiwa.
Tunatarajia litasaidia kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na kushughulikia changamoto zao kwa wakati,” alisema Mwang’onda.
Aidha, aliwataka wananchi kuendelea kudumisha amani, umoja na utulivu ili kuwezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa manufaa ya jamii.
Kwa mujibu wa taarifa ya mradi iliyosomwa na Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Sango, Seif Issa, ofisi hiyo itahudumia wakazi 5,806 wa kijiji hicho. Mradi umegharimu jumla ya Shilingi milioni 50.8.
Fedha zilizotumika kutekeleza mradi huo zilipatikana kutoka vyanzo mbalimbali, ambapo Shilingi milioni 1 zilichangwa na wananchi, Shilingi milioni 32.8 zilitokana na mapato ya kijiji, Shilingi milioni 7 zilitolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, huku Shilingi milioni 10 zikitolewa kupitia Mfuko wa Maendeleo wa Mwenge wa Uhuru.
Afisa Mtendaji huyo alieleza kuwa kukamilika kwa ofisi hiyo kutaboresha huduma za utawala, kurahisisha uhifadhi wa kumbukumbu na nyaraka muhimu, pamoja na kuongeza ushiriki wa wananchi katika shughuli za maendeleo ya kijiji.







