Mtu mmoja amefariki dunia na wengine saba kujeruhiwa kufuatia mlipuko wa baruti uliotokea leo alfajiri Julai 1, 2026 kwenye kibanda cha kuuzia kahawa kilichopo mtaa wa Sahwa ya Juu, Kata ya Lwanihma Wilayani Nyamagana Mkoani Mwanza.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza DCP Wilbrod Mutafungwa, aliyepoteza maisha katika tukio hilo ni Marco Msenyele Mfumadilu, maarufu kama Shija ambaye ni mkazi wa Lwanihma anayefanya kazi ya ulipuaji wa mawe kwa ajili ya kusafisha viwanja kabla ya kuanza ujenzi.
Mutafungwa amesema mlipuko huo umetokea majira ya saa 12.45 alfajiri kwenye kibanda cha kahawa kinachomilikiwa na Daud Joseph Baraka.
Ameongeza kuwa majeruhi miongoni mwa majeruhi wa tukio hilo wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando ( BMC ) jijini Mwanza pamoja na Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana Butimba.
Baadhi ya wakazi wa Mwanza wameeleza kusikitishwa na tukio hilo, wakisema wataendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kutoa taarifa kuhusu watu wanaotumia vilipuzi kwa ajili ya kulipua mawe katika maeneo yao bila kuwa na vibali halali ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao.







