Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amepongeza kiwango kikubwa cha ushiriki wa Watanzania katika utekelezaji wa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), akisema mradi huo umeendelea kuwa chanzo cha ajira, uhamishaji wa ujuzi na kukuza sekta binafsi nchini.

Akizungumza wakati wa mwendelezo wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya mradi huo katika Kituo cha Kupunguza Msukumo wa Mafuta cha Sindeni, wilayani Handeni mkoani Tanga, Waziri Ndejembi amesema ameridhishwa na ushirikishwaji wa Watanzania katika ngazi zote za utekelezaji wa mradi huo, kuanzia wahandisi hadi wafanyakazi wasio na ujuzi.

Amesema jambo lililomfurahisha zaidi ni kuona Watanzania wakishiriki kikamilifu katika kila hatua ya utekelezaji wa mradi huo, hali ambayo imewapa ujuzi na uzoefu wa kushiriki katika miradi mingine mikubwa ya kimataifa.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, mradi wa EACOP umezalisha jumla ya ajira 10,000, ambapo ajira 7,500 sawa na asilimia 75 zimetolewa kwa Watanzania. Amesema hatua hiyo imewajengea vijana uwezo wa kitaalamu na kuwapa uzoefu utakaowawezesha kushiriki katika miradi mingine ya kimkakati ndani na nje ya nchi.

Aidha, amesema licha ya mradi huo kufikia hatua za mwisho za utekelezaji, fursa za ajira na maendeleo ya kitaalamu zitaendelea kuwepo wakati wa uendeshaji wa bomba hilo, hivyo kuendelea kuwanufaisha Watanzania kwa muda mrefu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here