MOROGORO
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Kitila Mkumbo amesema Tanzania itajitosheleza kwa uzalishaji sukari kwa asilimia 100 ifikapo Juni 2026.
Alisema hatua hiyo itaondoa utegemezi wa kuagiza sukari kutoka nje ya nchi na badala yake nchi itazalisha sukari ya kutosha kwa matumizi ya ndani na ziada kwa ajili ya kuuza nje.
Mkumbo alitoa kauli hiyo wakati akikagua maendeleo ya miradi ya uwekezaji katika Shamba la Serikali la Mkulazi I, lililopo katika Kata za Matuli na Mkulazi, Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro.
Alisema mafanikio hayo yanatokana na mikakati ya serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi kuongeza uzalishaji wa sukari na kuimarisha sekta ya kilimo kwa ujumla.
Alisema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa inayolenga kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa chakula barani Afrika.
Aidha, alisisitiza kuwa serikali itaendelea kuwalinda wawekezaji wenye nia njema ya kuongeza tija na ajira ili kufikia lengo la kuwa na uchumi mkubwa katika kipindi cha miaka 25 ijayo kupitia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Alibainisha kuwa sekta ya kilimo ni miongoni mwa sekta tisa mama zitakazochochea ukuaji huo wa uchumi.
Mkumbo aliongeza kuwa Tanzania ina takribani hekta milioni 44 zinazofaa kwa kilimo lakini hadi sasa ni asilimia 30 tu ya eneo hilo linalolimwa. Alisema ni wakati wa kuachana na kilimo cha kujikimu na kuelekea kwenye kilimo cha kibiashara chenye tija zaidi.
Kwa mujibu wa waziri huyo, serikali inalenga kuendeleza kilimo cha aina mbili; kuwainua wakulima wadogo ili washiriki kikamilifu katika kilimo biashara na kuvutia wakulima na wawekezaji wakubwa watakaosaidia kuongeza uzalishaji na thamani ya mazao.
Akizungumza kwa niaba ya wawekezaji, Meneja Mkuu wa Santango Limited, Luab Luiz de Carvalho alisema licha ya uwekezaji mkubwa walioufanya katika miundombinu bado wanakabiliwa na changamoto ya baadhi ya wafugaji kuingiza mifugo katika mashamba yao hali inayorudisha nyuma jitihada za uzalishaji.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mussa Kilakala aliwahakikishia wawekezaji hao kuwa suala la ulinzi na usalama katika maeneo ya uwekezaji limepewa kipaumbele na hatua madhubuti zimeanza kuchukuliwa ili kuhakikisha shughuli za kiuchumi zinafanyika bila matishio yoyote.
