WENGI WASUMBULIWA NA MAUMIVU YA MIFUPA, VIUNGO

Date:

Share post:

RIPOTA PANORAMA

ASILIMIA 80 ya wagonjwa wanaofika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), wanasumbuliwa na maumivu ya mifupa na viungo.

Hayo yamesemwa hivi karibuni jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi wa MOI, ambaye pia ni Daktari bingwa mbobezi wa mifupa na uti wa mgongo, Dk. Anthony Assey, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kambi maalum ya matibabu itakayofanyika Februari 23 hadi 27, 2026, katika Hospitali ya Arusha Medical Centre – Selian.

Alisema wagonjwa wengi wanasumbuliwa na magoti, mgongo na nyonga ikilinganishwa na wanaofika kwa matibabu ya kansa au majeraha ya ajali.

Kati ya wagonjwa hao, asilimia 20 hadi 25 wanatoka mikoa ya Kaskazini, hasa Arusha.

Dk. Assey amesema ongezeko la maumivu ya mifupa na viungo linachangiwa na mabadiliko ya mtindo wa maisha kutokana na maendeleo ya kijamii, yakiwamo ulaji usiofaa unaosababisha uzito kupita kiasi, kutofanya mazoezi na matumizi ya vinywaji vyenye sukari, tumbaku na pombe.

Ameongeza kuwa kuongezeka kwa upatikanaji wa huduma na uelewa wa wananchi kumewafanya wengi kufika hospitalini kupata matibabu ikilinganishwa na kipindi cha nyuma.

“Nashauri watu kubadili mtindo wa maisha kwa kuzingatia lishe bora, kufanya mazoezi au kutembea mara kwa mara, kufanya kazi za mikono kama kulima bustani na kuacha uvutaji sigara pamoja na matumizi ya pombe na vinywaji vyenye sukari kwa wingi. Hii itasaidia kupunguza maumivu ya mifupa na viungo,” amesema Dk. Assey.

Amesema katika kambi hiyo, wataalamu wanatarajia kutoa huduma za kibingwa katika maeneo matano, ikiwemo matibabu ya majeruhi wa ajali waliovunjika mifupa, kunyoosha na kurekebisha mifupa, matibabu ya maumivu ya muda mrefu ya mgongo na shingo pamoja na ushauri kuhusu matatizo ya mifupa na magoti.

 Na watoto wenye matatizo ya mifupa ikiwamo kuzaliwa na miguu iliyopinda au maumivu ya muda mrefu pia watapatiwa matibabu stahiki.

Aidha, huduma za upasuaji wa ubongo zitatolewa kwa wagonjwa waliopata majeraha ya kichwa kutokana na ajali au wenye uvimbe huku wataalamu wakitoa ushauri na mapendekezo ya matibabu kulingana na hali ya mgonjwa kwa kutumia vifaa vya kisasa.

Dk. Assey amesema kutakuwa na wataalamu wabobezi katika upasuaji wa mifupa na viungo kwa watu wazima, ubadilishaji wa viungo vya nyonga na magoti, matibabu ya mifupa kwa watoto pamoja na daktari bingwa wa magonjwa ya kichwa na ubongo.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dk. Tatizo Wanne, amesema kambi hiyo ya upimaji wa mifupa, mishipa ya fahamu na ubongo inafanyika kwa ushirikiano wa madaktari wa Selian, MOI na JKCI ambayo inasimamia utendaji wa Hospitali ya Arusha Medical Centre – Selian.

Ameeleza kuwa kambi hiyo ni utekelezaji wa agizo la serikali la kusogeza huduma za afya karibu na wananchi ambapo upimaji utafanyika bure na wagonjwa watakaobainika kuhitaji matibabu watapatiwa huduma.

Ameongeza kuwa mkoa wa Arusha una uhitaji mkubwa wa huduma hizo hivyo wameamua kushirikiana na MOI kuleta huduma hiyo karibu na wananchi.

Amesema zaidi ya wataalamu 70 watashiriki kutoa huduma za matibabu na wanatarajia kuhudumia  wagonjwa zaidi ya 200 kwa siku, kulingana na mwitikio na hali ya utoaji wa huduma.

About The Author

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

spot_img

Related articles

UCHUMI WA CHINA WAZIDI KUIMARIKA

BEIJING, China LICHA ya vita vya Marekani na Iran kuonekana kuitikisa dunia, China imeendelea kupiga hatua kubwa katika eneo...

SIKU 100 ZA RAIS MPYA WA VENEZUELA: MABADILIKO NA MASWALI MAPYA

CARACAS, Venezuela BAADA ya vikosi vya Marekani kumng’oa madarakani aliyekuwa Rais wa Venezuela, Nicolás Maduro kwenye oparesheni ya Januari...

MAELFU YA FAMILIA SUDAN BADO WAKIMBIA VITA, HALI YA MAISHA YAZIDI KUWA MBAYA

MAELFU ya familia nchini Sudan bado wanalazimika kuyakimbia makazi yao, miji na hata mipaka ya nchi kufuatia vita...

ISRAEL YAENDELEA NA OPERESHEN DHIDI YA HEZBOLLAH NCHINI LEBANON

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema Jeshi la nchi yake linaendelea na operesheni dhidi ya wanamgambo wanaoungwa...