DAR ES SALAAM
MAMLAKA ya uteuzi imeiongezea muda wa siku arobaini na mbili (42) kuanzia Februari 20, 2026 Tume ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba, 2025.
Ongezeko hilo la muda linakusudia kuipa muda wa kukamilisha uchunguzi wa matukio ya uvunjifu wa amani ya wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025. Tume sasa inatakiwa kuwasilisha taarifa yake kabla au ifikapo Aprili 3, 2026.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa katika gazeti la serikali, tume imeongezewa muda ili kutoa fursa na muda wa kutosha kwa kila mwenye taarifa, ushahidi au maoni, aliyepo nchini au nje ya nchi kuuwasilisha kwa tume’
Kwamba ongezeko la muda pia linalenga kutoa nafasi kwa watu na au taasisi zenye taarifa na ushahidi ambao hawajafika mbele ya tume.
Sababu nyingine za kuongeza muda ni wingi na mchanganyiko wa taarifa zilizokusanywa na zinazoendelea kukusanywa na tume ambazo zinahitaji muda zaidi wa kufanyiwa uchambuzi wa kina/

Pia tume kulazimika kutumia wataalamu (experts) kutoka ndani na nje ya nchi wenye uwezo wa kufanya uchunguzi wa kisayansi na uchambuzi wa kidijitali wa baadhi ya taarifa na vielelezo kutokana na aina ya matukio na ushahidi uliokusanywa hadi sasa na unaoendelea kuwasilishwa.
Sababu nyingine ni tume kubaini mapengo kadhaa katika taarifa na vielelezo vilivyokusanywa hadi sasa hivyo kuhitaji kutafuta au kupata taarifa zaidi ili kukamilisha ushahidi kwa kila hoja inayohusika, kutoa fursa kwa wadau wachache muhimu ambao kwa sababu mbalimbali bado hawajafika mbele ya tume licha ya kupelekewa mialiko zaidi ya mara moja.
Taarifa hiyo imewataja wadau hao kuwa ni pamoja na baadhi ya viongozi wa dini, viongozi wa baadhi ya vyama vya siasa, taasisi na mashirika yasiyo ya kiserikali na watu binafsi na wingi wa wananchi wengine wanaoendelea kufika mbele ya tume kuwasilisha taarifa, ushahidi na ushauri wao.

Kutokana na fursa hiyo ya tume kuongezewa muda, mwenyekiti wakem, Jaji Othuman Chande imetoa wito kwa wananchi wote kuendelea kuwasilisha ushahidi kwenye tume kwa kutumia njia zote zilizoainishwa awali ambazo ni majadiliano ya ana kwa ana, mawasilisho ya maandishi (written submissions) kwa njia ya posta au tovuti maalumu ya tume; barua pepe; ujumbe mfupi wa simu (SMS); kujaza dodoso maalumu kwenye mtandao (www.tume.uchunguzi.go.tz), au kwa kupitia mitandao mingine ya kijamii.
Pia tume hiyo imetoa wito maalumu kwa baadhi ya viongozi wa dini, viongozi wa baadhi ya vyama vya siasa, taasisi na mashirika yasiyo ya kiserikali na watu binafsi ambao wamepewa mialiko na tume kutumia fursa hiyo kufika au kuwasiliana na tume kutoa mchango wao katika uchunguzi unaoendelea kwa manufaa ya wananchi, wadau na nchi kwa ujumla.
Awsali tume ilipaswa kuwasilisha taarifa kabla au ifikapo Februari 20, 2026 ikiwa ndani ya siku 90. Ilianza kutekeleza majukumu yake Novemba 20, 2025.
