Thursday, September 11, 2025
spot_img

DANIDA WAMWAGA MAPESA LSF

 

Balozi wa Denmark, Matte Norgaard Dissing-Spandet (kushoto) na Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Legal Servies Facility (LSF) Lulu Ng’wanakilala (kulia) wakibadilishana nyaraka za makubaliano baada ya tukio la kuweka saini mkataba wa ruzuku ya nyongeza, Shilingi Bilioni 5.6 zilizotolewa na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Denmark (DANIDA) kwa ajili ya mradi wa upatikanaji haki katikas kipindi cha mwaka mmoja.
 

MASHAKA MHANDO, TANGA

SHIRIKA la Maendeleo la Kimataifa la Denmark (DANIDA), limeipatia ruzuku ya kiasi cha shilingi 5.6 bilioni, ambazo ni sawa na Dola za Marekani Milioni 2.4, Shirika la Msaada wa kisheria (LSF) kwa ajili ya  kutekeleza mradi wa upatikanaji wa haki nchini. 

Mradi huo utakaotekelezwa kwa kipindi cha mwaka mmoja, kati ya Januari na Disemba 2021, ulisainiwa kati ya Mtendaji Mkuu wa LSF, Lulu Ng’wanakilala na Balozi wa Denmark hapa nchini Mette Norgaard Dissing-Spandet.   

Akizungumza katika hafla fupi ya kukabidhi mkataba wa kukabidhi ruzuku hiyo, Ng’wanakilala alisema wamepokea ruzuku hiyo ikiwa ni nyongeza ya kutekeleza mradi wa upatikanaji wa haki unaolenga kuboresha mazingira ya uwezeshaji wa kisheria nchini. 

“Tutazijengea uwezo taasisi zinazotoa huduma ya msaada wa kisheria pamoja na huduma za wasaidizi wa kisheria nchini kwa makundi mbalimbali katika jamii hususani wanawake na watoto, ” alisema.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Legal Services Facilities (LSF) Lulu Ng’wanakilala, akisaini mkataba wa ruzuku ya nyongeza ya Shilingi Bilioni 5.6 zilizotolewa na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Denmark (DANIDA) kutekeleza mradi wa upatikanaji haki 



Alisema mradi huo unalenga kujenga msingi endelevu wa huduma za msaada wa kisheria  kupitia upya mifumo, sera na sheria mbalimbali kandamizi zinazorudisha nyuma ustawi na maendeleo ya wanawake na watoto katika jamii kwa lengo la kuboresha mifumo ya upatikanaji wa haki nchini katika ngazi mbalimbali.

Alisema mradi huo unafanyika nchini Tanzania ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa malengo mawili endelevu ikiwemo lengo namba tano (SDG5) na namba 16 (SDG16), ambayo yanaangazia masuala ya usawa wa kijinsia na uwezeshwaji wa wanawake pamoja na kukuza upatikanaji wa haki kwa watu wote.

“Mradi huu ni sehemu ya utekelezaji wa dira ya maendeleo nchini Tanzania ifikapo mwaka 2025, ambayo inatambua umuhimu wa masuala ya usawa kama njia ya kujenga msingi wa amani na utawala bora, ambavyo vyote vinachangia kwa kiasi kikubwa kufikia mifumo endelevu ya upatikanaji wa haki nchini, ” alisema Ng’wanakilala. 

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Mette Norgaard Dissing-Spandet alisema, DANIDA imeamua kuwaongezea ruzuku LSF kwa kipindi cha mwaka mmoja ikiwa ni sehemu yake ya uwajibikaji katika kuhakikisha suala la upatikanaji wa haki nchini Tanzania linazingatiwa.

“LSF ni mdau wetu mkubwa kwa takribani miaka 10 sasa, ambapo amekuwa akifanya kazi kubwa nchini Tanzania.  Tumeamua kuongeza kiwango hiki cha ruzuku ili kusaidia zaidi utekelezaji wa mradi unaotekelezwa na LSF kwa ajili ya maendeleo ya kina mama na watoto ambao ndio wahanga wakubwa wa masuala ya haki zao. 

“Aidha, tunaamini ruzuku hii itasadia kuboresha mifumo ya utoaji haki iliyo rasmi na isiyo rasmi ili kuwezesha upatikanaji wa haki kwa wakati. 

“Lakini pia kuwezesha upatikaji wa sera na sheria bora zinazolinda maslahi ya watanzania wote hususani wanawake na watoto. Ufadhili huu ni sehemu yetu katika kuhakikisha kuwa jamii yote nchini Tanzania inakuwa na utawala wa sheria unaoheshimu kila mtu bila kujali umri au jinsia,” alisema balozi huyo.

Balozi wa Denmark, Matte Norgaard Dissing-Spandet akitia saini mkataba wa ruzuku ya Shilingi Bilioni 5.6 zilizotolewa na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Denmark (DANIDA) kwa Shirika la Legal Services Facilities kwa ajili ya kutekeleza mradi wa upatikanaji haki



Akitoa neno la shukrani, Lulu Ng’wanakilala, alisema ruzuku iliyotolewa na wadau hao itasaidia kikamilifu kuendelea kutekeleza mradi wa upatikanaji wa haki nchini unaotekelezwa nchi nzima kwa upande wa Tanzania Bara na visiwani Zanzibar. 

“Ikumbukwe kwamba miezi sita iliyopita, DANIDA walitoa ruzuku kwa LSF ya kiasi cha shillingi milioni 719,500,000 ambazo ni sawa na Dola za Marekani Milioni 311,471.86 ili kuwezesha elimu ya mpiga kura na usimamizi wa uchanguzi kwa mashirika  31 yaliyopewa vibali na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuendesha shughuli hizo za uchaguzi, ” alisema. 

Ng’wanakilala aliongeza kuwa, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita LSF imekuwa ikishirikiana na wadau wake mbalimbali ikiwemo DANIDA, ambapo imeweza kusaidia kuboresha sekta ya msaada wa kisheria nchini kupitia uwezeshaji wa kisheria kwa kuyapa ruzuku mashirika zaidi ya 200 yanayotoa huduma za msaada wa kisheria pamoja na huduma za watetezi wa kisheria nchini kote;

“Ufadhili huu utaendelea kuwezesha upatikanaji wa huduma za msaada wa kisheria bure katika wilaya zote Tanzania Bara na Zanzibar kupitia wasaidizi wa msaada wa kisheria zaidi ya 4000 nchi nzima.

“Hivyo Tunawashukuru sana wadau wetu DANIDA kwa kuendelea kutusaidia katika utekelezaji mradi wetu wa upatikanaji wa haki nchi nzima. Kwa takribani miaka 10 sasa DANIDA wamekuwa na mchango mkubwa katika kuhakikisha mradi wetu huu unawanufaisha wananchi wengi nchini hususani wanawake na watoto.

“Mwaka 2020, tumeweza kuwapatia msaada wa kisheria watu takribani 99,844, ambapo wanaume pekee walikuwa 39,641 sawa na asilimia 40, huku wanawake wakiwa ni 60,203 sawa na asilimia 60.  Mashauri yanayofikishwa kwa wasaidizi wa kisheria ni pamoja na migogoro ya ardhi, ndoa, mirathi, matunzo kwa watoto, pamoja na vitendo vya ukatili wa kijisia. Kati ya mashauri yaliyoripotiwa kwa wasaidizi wa kisheria asilimia 66 yalitatuliwa,”  alisema Ng’wanakilala.

 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya