![]() |
Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kipolisi Kinondoni (RPC) Ramadhani Kingai (aliyesimama mbele) |
MWANDISHI WA PANORAMA
KUNA utata wa namna Jeshi la Polisi, Mkoa wa Kipolisi Kinondoni lilivyochunguza na kuchukua hatua dhidi ya watuhumiwa saba waliokamatwa na bangi nyumbani kwa Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Magereza, Ramadhani Nyamka.
Tangu kukamatwa kwa watuhumiwa hao wakivuta bangi na wakiwa na bangi nyumbani kwa Kamishana Msaidizi Mwandamizi Nyamka, Kinondoni, Dar es Salaam, na pia kukuta bangi ikiwa inastawishwa uani mwa nyumba hiyo, Jeshi la Polisi Kinondoni limekuwa na kigugumizi kuzungumzia mwenendo wa uchunguzi lilioufanya na matokeo yake.
Aidha, ikiwa imepita miezi zaidi ya sita sasa tangu tukio hilo lilipotekea, Jeshi la Polisi Kinondoni limeshindwa kusema iwapo lilimuhoji Kamishna Nyamka ambaye pia ni Kamishna wa Utawala na Rasilimali Watu wa Jeshi la Magereza kuhusu nyumba yake kukutwa ikiwa inastawisha bangi uani.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni (RPC), Ramadhani Kingai ambaye mara kadhaa alizozungumzia tukio hilo amekuwa hana majibu ya moja kwa moja na ya kina, tofauti na ambavyo imekuwa ikitokea katika matukio mengine; mbali ya hilo, aliwaruhusu watuhumiwa hao wa matumizi ya mihadarati ambao mwaka jana walipokamatwa walikuwa wanafunzi wa kidato cha nne, kwenda kufanya mitihani ya kumaliza elimu ya Sekondari.
Wakati watuhumiwa hao wa mihadarati wakiruhusiwa na Jeshi la Polisi kufanya mitihani, mtuhumiwa mwingine wa kubaka na kumtorosha kutoka shuleni mwanafunzi wa kidato cha tatu wa Shule ya Sekondari ya St, Mary’s, Rahim Nyamka ambaye ni mtoto wa Kamishna Nyamka naye aliachwa aendelee na maisha yake huku mwanafunzi aliyemtorosha, kumbaka na kumvutisha bangi akiwa hafahamiki alipo.
![]() |
Wakili Kiongozi wa Kampuni ya Uwakili ya Haki Kwanza, Aloyce Komba |
Kwa mujibu wa vifungu namba 11(1) na (2) na 15(1) na (2) vya sheria ya udhibiti wa dawa za kulevya ya mwaka 2019, sura ya 95, kama vinavyoelezewa na Wakili Kiongozi wa Kampuni ya Uwakili ya Haki Kwanza, Aloyce Komba, vinasema;
‘Mtu yoyote anayelima mmea uliokatazwa au anazalisha mbegu za mmea huo kwa lengo la kutengeneza dawa za kulevya, mtu huyo anaweza akawa ndiye mmiliki wa ardhi au nyumba anayoishi au ameipangisha kwa ajili ya kilimo cha mmea uliokatazwa kwa ajili ya kuzalisha dawa za kulevya.
‘Mtu huyo atakuwa ametenda kosa la jinai ambalo akitiwa hatiani, atapewa adhabu ya kifungo isiyopungua miaka thelathini.’
Wakili Komba anafafanua kuwa; “Kulima ni pamoja na kukusanya kilicholimwa na katika shauri hilo kuna mambo mawili, mosi ni kosa la kulima (planting) bangi na pili, kukutwa nayo (posession of norcotics). Kama ingekuwa imeshavunwa kosa linaangalia uzito ni kilo ngapi. Misokoto inapimwa, ikizidi gram 20, hakuna dhamana.”
Kwa mujibu wa RPC Kingai, tayari majalada mawili ya uchunguzi wa matukio ya kubaka na kupatikana na bangi yamekwishapelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa ajili ya hatua zaidi lakini polisi wamekuwa wakisita kuongelea uchunguzi na ripoti ya uchunguzi wa majalada hayo.
![]() |
Bangi |
Hivi karibu, RPC Kingai alipoulizwa hilo kutokana na maswali yasiyokuwa na majibu yaliyoibuka baada ya kuripotiwa kwa matukio hayo alisema hana uhakika watuhumiwa hao saba walikutwa na gramu ngapi za bangi na pia hana uhakika iwapo Kamishna Nyamka alihojiwa baada ya nyumba yake kukutwa ikistawisha bangi.
Watuhumiwa saba wa mihadarati, walikamatwa na timu maalumu iliyoundwa na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, ambaye sasa ni Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongoli kumsaka mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya St, Mary’s, Lubna Said aliyekuwa ametoroshwa shuleni na mtoto wa Kamishna Nyamka na wakati wa ukaguzi ndani ya nyumba hiyo walikutwa wakivuta bangi na nyingine wakiwa nayo; na baada ya nyumba hiyo kukaguliwa zaidi ndipo iligundulika kustawishaji wa bangi uani.
Taarifa za kukamatwa kwa watuhumiwa hao zilitolewa Mwenyekiti wa Timu ya Uchunguzi ya Chongolo, Joseph Kapere na baadaye kuthibitishwa na RPC Kingai.
Akithibitisha kuwepo kwa tukio hilo Oktoba mwaka jana, RPC Kingai alisema watuhumiwa hao ni wanafunzi hivyo Jeshi la Polisi limewaachia kwa ruhusa ya kiutu, kwenda kufanya mtihani wa kidato cha nne kwa sababu ni wanafunzi na watakapomaliza ndipo hatua za kisheria dhidi ya tuhuma zinazowakabili zitachukuliwa.
Hata hivyo, katika mahojiano ya awali ambayo RPC Kingai alifanya na Tanzania PANORAMA, alikataa kutaja majina ya watuhumiwa na jina la mmiliki wa nyumba walimokamatwa, lakini baadaye katika uchunguzi wake Tanzania PANORAMA ilibaini kuwa nyumba hiyo ni mali ya Kamishna Msaidizi Mwandamizi Nyamka.
Mwenyekiti wa Kamati ya Chongolo, Kapere, amepata kuiambia Tanzania PANORAMA kuwa kubainika kwa vijana hao na nyumba hiyo kulitokana na hatua ya Mkuu wa Shule ya Sekondari ya St. Mary’s, Ntipoo Yissambi kuipeleka timu ya uchunguzi katika nyumba aliyokuwa akiishi mwanafunzi Lubna na mpenzi wake Rahim baada ya kutoroshwa shuleni.
Naye Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Nyamka katika mahojiano aliyopata kufanya na Tanzania PANORAMA kuhusu nyumba yake kustawisha bangi na kuishi vijana wanaotumia bangi, aling’aka kwa ukali na kuhoji kwa nini habari hiyo iliandikwa bila kwanza yeye kutafutwa.
“Unasema nani? Ndiyo wewe wa Tanzania PANORAMA. Nyamaza kwanza, nataka uniambie ni kwanini aliandika hizo habari bila kunitafuta kwanza. Eeeeeh, nambie, ni kwanini,,,,,?” aling’aka Kamishna Nyamka.
Tmu ya uchunguzi ya Chongolo ambayo ilikwishakamilisha kuandika ripoti yake ambayo Tanzania PANORAMA imeiona, ilieleza kubaini Mwanafunzi Lubna alitoroshwa na Rahim Nyamka, usiku wa Oktoba 4, 2020 ambaye alimpeleka katika nyumba ya baba yake, Kamishna Nyamka ambako pamoja na mambo mengine alimwingilia kimwili na kumvutisha bangi.
Taarifa za kutoroshwa kwa mwanafunzi Lubna zilifichwa na uongozi wa Shule ya Sekondari ya St Mary’s hadi ziliporipotiwa katika Kituo cha Polisi cha Stakishari na wazazi wake na kupewa RB STK/RB/10714/2020 na jalada la upelelezi wa kesi hilo lilikabidhiwa kwa Askari Polisi Mpelelezi, Gwake Mwakapande.