![]() |
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,Nape Nnauye akizungumza jana wakati akifungua kikao cha 17 cha maafisa habari nchini kinachofanyika mkoani Tanga |
RIPOTA MAALUMU
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ameagiza utengenezwe utaratibu wa mafunzo kwa maafisa habari nchini juu ya miradi mikubwa ya kitaifa inayotekelezwa na Serikali ili wawe na uelewa wa kuisemea miradi hiyo wakati wowote.
Aliyasema hayo jana alipokuwa akifungua kikao cha 17 cha maafisa habari, mawasiliano na uhusiano wa Serikalini kinachoketi kwa siku tano jijini Tanga.
Alisema lazima maafisa habari wawe wanajua miradi inayotekelezwa kwenye maeneo yao ili waweza kujua namna ya kuielezea kwa wananchi.
Nape alisema wananchi wanafahamu ndani mwaka mmoja, Rais Samia Suluhu Hassan ameleta mageuzi makubwa hivyo ni jukumu la maafisa habari wa Serikali kuhakikisha hata wanapoamshwa usingizini wawe wanajua mambo yanayoendelea ndani ya Serikali.
Aliwataka maafisa habari waliopo mikoani kuchukua muda wa kuelewa miradi inayoendelea kwenye maeneo yao ili wawe na jambo la kusema.
Akitoa mfano, alisema Afisa Habari wa Mkoa wa Tanga anapaswa kufahamu kwa kina mpango wa kuwahamisha watu kutoka Ngorongoro kuja Msomera wilayani Handeni.
Aliagiza uandaliwe mjadala ya maafisa habari kwa kutumia teknolojia ya kisasa ili kupunguza gharama kubwa ya kufanya majadiliano ya pamoja, jambo ambalo alisema linawezekana.
Aidha, Nape alitoa siku 14 kwa maafisa habari nchini kuhakikisha kila tovuti ya Serikali inakuwa na taarifa zinazoendana na wakati na alionya kuwa atawashughulikia watakaoshindwa kutekeleza agizo hilo.
Aliwataka maafisa habari wa Serikali kutoruhusu watu wapotoshe mafanikio ya Serikali na badala yake wajibu hoja ili kuwaelewesha wananchi.
Alisema kuna tatizo sugu katika tovuti na mitandao ya kijamii ya wizara na taasisi mbalimbali za Serikali kuwa na habari zilizopitwa na wakati.
“Nitoe siku 14 kuanzia tarehe 14 Mei, kila tovuti ya Serikali au taasisi ya Serikali au Serikali za Mitaa iwe na taarifa zinazoendana na wakati. Afisa habari atakayeshindwa kutekeleza hili ndugu Msigwa hatutaweza kuendelea naye inabidi tuachane naye,” alisema Nape.
Alisema anajisikia vibaya anapopita na kusikia kuna taasisi za Serikali tovuti za mkoa za wizara, wilaya au halmashauri zina taarifa za miaka miwili au mitatu iliyopita.
“Halafu tuna afisa habari kwenye hilo eneo, haiwezekani jamani na tusipoambiana tutakuwa hatutendeani haki jamani sasa siku 14 zinatosha kabisa Msigwa ulikague na nipate taarifa ya jambo hili.
![]() |
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk. Jimmy Yonazi akizungumza jana katika kikao kazi cha maafisa habari wa Serikali kilichoanza jana mkoani Tanga. |
“Nasikitika kuona tovuti ya wilaya, mkoa, halmashauri haziendani na wakati. Watu wengi wameacha kutembelea tovuti za Serikali kwa ajili ya kuwepo taarifa zilizopitwa na wakati, umefika wakati sasa tutoke kwenye aibu hiyo imewafanya watu hawatembelei tovuti za Serikali wakati kuna maafisa habari.
“Mhakikishe mnajibu hoja za wananchi kwenye vyombo vya habari kwa wakati muafaka kuhusu changamoto zinazojitokeza, msiruhusu watu wapotoshe ukweli kwani ukweli unapopotoshwa ni aibu kwa maafisa habari.
“Supu inanywewa ya moto, usisubiri mpaka usukumwe kwenda kukanusha habari ambayo ni ya uongo akikubip saa moja, saa mbili nawe sema tukienda hivyo watakuwa na nidhamu kwenye kupotosha,” alisistiza Nape.
Katika hatua nyingine Waziri Nape ameahidi kupeleka maafisa habari katika mikoa 7 ambako hawapo. Aliitaja mikoa hiyo kuwa ni Manyara, Lindi, Mbeya, Tabora, huku akiijumuisha pia mikoa ya Kigoma, Dodoma na Geita ambayo maafisa habari wake wamekuwa wasaidizi wa wakuu wa mikoa.
![]() |
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa akizungumza jana katika kikao cha maafisa habari wa Serikali kinachofanyika mkoani Tanga. |
Awali akizungumza katika kikao hicho, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jimmy Yonazi alisema tasnia ya mawasiliano ya umma ni ya zamani na ni muhimu kwa sababu ndio imeandika historia ya Serikali juu ya namna inavyohudumia wananchi katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kimaendeleo.
Awali, Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa alisema maafisa habari wamepewa heshima kubwa na Rais Samia hivyo wana deni kubwa la kulipa kwa kufanya kazi bila kuchoka usiku na mchana kwa kuzingaia uadilifu, ubunifu na mabadiliko yanayotokea kila uchwao katika sekta hiyo nchini.
![]() |
Mwenyekiti wa Maafisa Habari Tanzania, Pascal Shelutete akizungumza jana katika kikao cha maafisa habari wa Serikali kinachofanyika mkoaniTanga |
Mwenyekiti wa maafisa habari nchini, Pascal Shelutete alimshukuru Waziri Nape kwa kuwa mgeni rasmi katika kikao hicho huku akiahidi kuwa; kwa maafisa habari wa Serikali, hotuba ya waziri ni maelekezo hivyo katika siku tano watakazokuwepo jijini Tanga watahakikisha wanaweka mikakati madhubuti ya kuyafanyia kazi maelekezo yote.