Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi, Bi. Zuwena Omary, amesema mkoa huo unaendelea kunufaika na utekelezaji wa afua za afya na usafi wa mazingira (WASH), hatua inayochangia kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
Ameyasema hayo Aprili 17, 2026 wakati wa ufunguzi wa kikao cha utekelezaji wa afua hizo kilichowakutanisha Waganga Wakuu wa Wilaya, Maafisa Afya na Mazingira pamoja na wadau wa sekta ya afya, Bi. Omary alisisitiza umuhimu wa kuongeza juhudi na uwajibikaji ili kuimarisha huduma za afya.
Aidha ameeleza kuwa utekelezaji wa mradi wa WASH umeleta mafanikio makubwa ikiwemo kuongezeka kwa upatikanaji wa maji safi, kuboreshwa kwa mazingira, pamoja na kupungua kwa magonjwa ya mlipuko. Aidha, umechangia kuhamasisha lishe bora na matumizi sahihi ya vyoo.
Kwa mujibu wa Bi. Omary, upatikanaji wa vyoo umeongezeka kutoka asilimia 56 hadi 64, huku vituo vya afya 117 vikifaidika na maboresho hayo. Alisisitiza pia umuhimu wa kufanya tathmini za mara kwa mara na kuweka mikakati madhubuti ya kuendeleza ubora wa huduma.
Pia aliwataka wakurugenzi wa halmashauri na wataalamu wa afya kuhakikisha taarifa za utekelezaji zinawasilishwa kwa wakati pamoja na kuimarisha ukaguzi wa biashara za chakula, hatua itakayosaidia kuongeza mapato kupitia sekta ya afya.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa, Dkt. Kheri Kagya, alisema mradi huo umeleta mafanikio makubwa, na baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza, awamu ya pili inatarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha 2026/2027. Alibainisha kuwa kila halmashauri itapatiwa shilingi milioni 161 kwa ajili ya kuendeleza utekelezaji wa afua hizo.






