Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amewasili mkoani Arusha kwa ziara ya kikazi ya siku mbili, akilenga kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo.
Dkt. Nchemba aliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Arusha leo Aprili 17, 2026, ambapo alipokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Nurdin Babu, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla.
Katika siku ya kwanza ya ziara yake, Waziri Mkuu anatarajiwa kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu wa AFCON 2027, pamoja na miradi ya miundombinu ikiwemo ujenzi wa Barabara ya Mzunguko (Ring Road) kipande cha Mbauda – Oljoro hadi eneo la Fun Retreat, jijini Arusha.
Aidha, katika siku ya pili ya ziara hiyo, Aprili 18, 2026, Dkt. Nchemba atakuwa mgeni rasmi katika mkutano wa Wafanyabiashara Wadogo na wa Kati (SMEs), utakaofanyika katika Hoteli ya Four Point, jijini Arusha.
Ziara hiyo inalenga kuhimiza utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na kukuza shughuli za kiuchumi katika mkoa wa Arusha na maeneo ya jirani.






