WASHINGTON DC, Marekani
AKIZUNGUMZA na waandishi wa habari Aprili 16, 2026, Rais wa Marekani, Donald Trump, alisema ana matumaini ya kuona wakifikia makubaliano katika mazungumzo ya pili kati yao na Iran.
Mazungumzo ya kwanza yaliyofanyika Aprili 12, 2026 hayakuzaa matunda baada ya pande mbili hizo kutokukubaliana katika baadhi ya mambo.
Moja ya masuala yaliyokuwa gumzo mezani ni mpango wa nyuklia, ambapo Iran iliripotiwa kugomea agizo la Marekani la kuitaka kuachana nao.
Sasa, wawakilishi wa Marekani na Iran watakutana tena wikiendi hii katika Hoteli ile ile ya Serena mjini Islamabad, Pakistan, wakijaribu kutafuta suluhu ya vita vyao vilivyodumu kwa wiki sita tangu vilipoanza Februari 28, 2026.
Rais Trump amedai kuwa Iran imebadili baadhi ya misimamo yake kuelekea Mkutano huo, ikiwamo kuahidi kutomiliki silaha za nyuklia kwa kipindi cha miaka 20 ijayo.
Pia, kwa mujibu wake, Iran imekubali kuwapa Marekani mavumbi yatokanayo na urutubishaji wa urani, ambayo hutumika kutengeneza silaha za nyuklia.
“Iran wanataka mazungumzo yapate suhulu. Wamekubali mambo ambayo hawakuwa wakikubaliana nayo miezi miwili iliyopita,” amesema.
Anaamini kuwa endapo Marekani na Iran zitafikia mwafaka na kumaliza kabisa mgogoro wa Mashariki ya Kati, bei ya mafuta na mfumuko wa bei utashuka.
Hata hivyo, wakati Rais Trump akiwa na matumaini makubwa, hali inayoonekana Iran inatoa picha tofauti na ya kutia shaka.
Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Bagher Ghalibaf, ambaye ni mwakilishi katika mazungumzo na Marekani, amesema Iran itakubali mwafaka endapo washirika wake wataheshimiwa na kuhusishwa katika mchakato wa kupatikana kwa suluhu.
Washirika anaowazungumzia Ghalibaf ni Hezbollah, Houthis na Hamas, ambavyo ni vikundi vyenye ‘sura ya ugaidi’ katika macho ya watawala wa Marekani na mataifa ya Magharibi.
Msisitizo wa Ghalibaf ni kwamba endapo Marekani na Israel zitachagua amani, basi ziache mashambulizi dhidi ya vikundi hivyo vya Lebanon, Yemen na Ukanda wa Gaza.
Ikumbukwe, Rais Trump amesisitiza mara kadhaa kuwa Hezbollah si sehemu ya mazungumzo ya amani ya Islamabad, licha ya kwamba Iran ilisema inataka kuona Israel ikiacha kulishambulia Kundi hilo.
Kwa mazingira hayo, Conrad Schetter, mtafiti wa masuala ya migogoro, anasema hatarajii makubwa katika duru ya pili ya mazungumzo kati ya Marekani na Iran.
Je, hofu yake inatokana nini? “Bado kuna hali ya kutokuaminiana. Iran haiamini kama Marekani ina nia njema, kama ambavyo na wenzao wanafikiria pia,” anasema Schetter.
Anaongeza kuwa vita vya wiki sita dhidi ya Marekani vimeiimarisha zaidi Iran kwa kuiongezea hali ya kujiamini.






