SERIKALI INATAFUTA NJIA MBADALA ZA KUPUNGUZA GHARAMA ZA MAISHA – MAJALIWA

Date:

Share post:

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa



*Aitisha kikao cha kutathmini bei ya mafuta

RIPOTA WA WAZIRI MKUU

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali inaendelea kutafuta njia mbadala ambazo zitapunguza gharama ya maisha kwa Watanzania kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia.

“Nawaomba Watanzania waendelee kuwa watulivu na waiamini Serikali yao kuwa tunaendelea kufanya kila linalowezekana ili kuhakikisha tunapunguza gharama za maisha kwa wananchi,”  alisema.

Waziri Mkuu Majaliwa alitoa wito huo leo Mei 5, 2022 katika kikao kilichofanyika ofisi ndogo ya Waziri Mkuu iliyoko Oysterbay, jijini Dar es Salaam ili kufanya tathmini ya bei ya mafuta na kuangalia namna gani Serikali inaweza kufanya ili kupunguza athari ya bei ya mafuta na kuleta unafuu wa gharama za maisha kwa Watanzania.

Waziri Mkuu alisema kikao hicho kimefanyika ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye aliagiza viongozi wa sekta husika wahakikishe wanatafuta suluhisho la kupanda kwa bei ya mafuta hata kama bei hiyo inaendelea kupanda duniani.

“Mheshimiwa Rais ameona changamoto wanayopitia Watanzania kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia, hivyo kikao hiki ni matokeo ya maagizo yake ya kuhakikisha sisi kama viongozi tunatafuta suluhisho la muda mfupi na la muda mrefu ili kukabiliana na changamoto hii,” alisisitiza.

Waziri Mkuu alisema kuwa tayari Wizara ya Nishati imeanza kutafuta njia mbadala za uagizaji wa mafuta pamoja na kupunguza makato mengineyo ili kupunguza bei ya mafuta.

“Serikali inaangalia njia mbadala za uagizaji wa mafuta, kupitia kwa wazabuni wengine kama ambavyo imeshauriwa na wabunge na tayari mchakato huo umeanza kwa kutathmini maombi 24 ambayo yaliwasilishwa kwa wizara na sasa wamebaki wazabuni sita ambao wameingia hatua inayofuata. Inachokifanya Serikali hivi sasa ni kujiridhisha na uwezo wao wa kusambaza mafuta kulingana na mahitaji na taratibu zilizowekwa na Serikali,” alisema.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), George Simbachawene, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Nishati, January Makamba, Makatibu Wakuu pamoja na watendaji wakuu wa taasisi za EWURA, TPDC na Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA).

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

spot_img

Related articles

NEWCASTLE KUMUUZA MSHAMBULIAJI WA BEI MBAYA

LONDON, UingerezaKLABU ya Newcastle United itampiga bei straika raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Yoane Wissa,...

LIVERPOOL NAYO YAJITOSA KWA WHARTON

MERSEYSIDE, UingerezaLIVERPOOL imeungana na klabu zingine kubwa za Ulaya zinazomtolea macho kiungo wa Crystal Palace, Adam Wharton. Mtandao wa...

SINTOFAHAMU KUELEKEA MAZUNGUMZO YA PILI KATI YA MAREKANI, IRAN

WASHINGTON DC, MarekaniAKIZUNGUMZA na waandishi wa habari Aprili 16, 2026, Rais wa Marekani, Donald Trump, alisema ana matumaini...

TAJIRI WA MAN CITY ANAHUSIKA VIPI VITA NCHINI SUDAN?

MANCHESTER, UingerezaMMILIKI wa klabu ya Manchester City, Sheikh Mansour bin Zayed Al-Nahyan, anakabiliwa na tuhuma nzito za kusambaza...