Â
*Shirika la Makazi Afrika lakubali kutoa mkopo kujenga nyumba za gharama nafuu
*Ofisi za UN Habitat kurejeshwa Tanzania
RIPOTA MAALUMU, KETOWICE POLAND
THAMANI ya mtaji wa nyumba za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), sasa imefikia Shilingi trilioni 5.4.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Fedha wa NHC, Adolph Kasegenya katika kikao baina ya NHC na ujumbe wa Shirika la Makazi Afrika (Shelter Afrique) juzi, Juni 28, 2022 katika Jiji la Ketowice, Poland ambako kongamano la 11 la miji duniani linafanyika.
Katika kikao hicho, ujumbe wa NHC uliongozwa na Balozi wa Tanzania nchini Kenya ambaye pia ni Mwakilishi wa Kudumu wa Shirika la Makazi Duniani ( UN Habitat) lenye Makao Makuu jijini Nairobi, Kenya, Dk. John Stephen Simbachawene.
Kasegenya alisema mtaji wa nyumba wa NHC unaofikia Shilingi trillion 5.4 unaliwezesha kukopesheka na uongozi mpya wa NHC unalenga kuwezesha ujenzi wa miradi ya nyumba za gharama nafuu kwa watu wa kipato cha kati na chini ili kutoa fursa kwa Watanzania kumiliki nyumba lakini changamoto iliyopo ni kupata fedha za kugharamia miradi hiyo.
Alisema NHC imeuona umuhimu wa kuzungumza na Shirika la Makazi Afrika ili lipate mkopo wenye riba na masharti nafuu utakaowezesha kutimiza malengo yake ya kujenga nyumba za gharama nafuu na kwamba mazungumzo kuhusu mkopo huo yalikwishaanza na sasa umefika wakati wa kuyakamilisha.
Akijibu hoja na maombi ya NHC, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Shirika la Makazi Afrika, Kingsley Muwowo alisema shirika hilo linaliamini NHC kwa sababu linalipa vizuri mikopo yake na hivi sasa halina deni.
Muwowo alisema kwa kuwa NHC lina ardhi na soko la uhakika la nyumba za gharama nafuu, Shirika la Makazi Afrika liko tayari kukamilisha mazungumzo yaliyokwishaanza kabla ya Septemba, 2022 ili liweze kupata mkopo linaouhitaji.
Kwa upande wake Balozi wa Tanzania nchini Kenya Dk. Simbachawene alilishukuru Shirika la Makazi Afrika kwa kuonyesha nia ya kuisaidia Tanzania kujenga nyumba bora za gharama nafuu na alitoa mwaliko kwa wajumbe wa shirika hilo kutembelea Tanzania ili kukutana na NHC na kuona miradi inayohitaji kupatiwa msukumo wa haraka. Mwaliko huo ulikubaliiwa na Shirika la Makazi Afrika.
Wakati huo huo, Shirika la Makazi Duniani limekubali ombi la Tanzania la kurejesha ofisi za shirika hilo Tanzania.
Ombi hilo la Tanzania lilitolewa mapema leo na Balozi wa Tanzania nchini Kenya ambaye pia ni Mwakilishi wa Kudumu wa Shirika hilo, Dk. John Simbachawene wakati wa kikao cha pamoja kati ya Mradi wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP), Shirika la Makazi Duniani (UN- Habitat) na Ujumbe wa Tanzania unaoshiriki Kongamano la 11 la Miji Duniani linalofanyika katika Jiji la Ketowice, Poland.
Akijibu ombi hilo la Tanzania, Mkurugenzi wa Shirika la Makazi Duniani, Kanda ya Afrika, Oumar Sylla alisema sera nzuri na uongozi bora wa Rais Samia Suluhu Hassan unaipa moyo taasisi hiyo ya makazi duniani kuzirejesha ofisi hizo nchini Tanzania.
Sylla alisema shirika hilo linaitambua Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zitakazokuwa na idadi kubwa ya watu duniani katika miaka ijayo, hivyo ni umuhimu kuwa na ofisi yake itakayoratibu na kusimamia changamoto za makazi, ukuaji wa miji na idadi kubwa ya watu.
Alisema Serikali ya Tanzania inatakiwa kuandaa mazingira ya kuanzishwa tena kwa ofisi hiyo katika ardhi yake.
Naye, Mratibu Mwandamizi wa Miradi ya Uendelezaji Makazi wa Shirika la Makazi Duniani, Kanda ya Afrika, Ishaku Maitumbi alisema Shirika hilo kwa kushirikiana na UNDP, limesaidia baadhi ya Serikali za Mitaa nchini ambazo tayari zina mipango ya vipaumbele vya maendeleo na mipango miji kuzijengea uwezo na kuibua miradi.
Alisema jumla ya Dola za Marekani milioni 30 zinatumika kugharamia miradi katika Halmashauri za Serikali za Mitaa 15 zilizopo mikoa sita ambayo ni Dodoma, Mara, Mwanza, Simiyu, Tanga na Mtwara.
Maitumbi alivitaja vigezo vilivyotumika kutoa misaada kwa Halmashauri hizo kuwa ni kiwango cha umaskini na mahitaji yake, uwezo wa kutekeleza miradi katika mikoa husika na uwezekano wa miradi iliyowekezwa kuwa endelevu.
Mkuu wa Utafiti wa UNDP Tanzania, Godfrey Nyamrunda ambaye pia alipata fursa ya kuzungumza alisema, miradi hiyo ina manufaa makubwa na alizitaka Mamlaka za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kusimamia kikamilifu miradi inayosaidiwa na taasisi hizo mbili ili iweze kuwa na manufaa kwa nchi.
Akizungumza katika kikao cha leo, Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Dk. Abdallah Possi alisema ili miradi inayosaidiwa iweze kuwa na manufaa ni lazima wanaoisimamia wajengewe uwezo na uelewa hususan unaohusu miji na makazi.
Kongamano la Miji Duniani linafanyika jijini Ketowice Poland likiwa na washiriki wapatao 25,000 kutoka mataifa mbalimbali duniani na kwa sehemu kubwa linajadili changamoto za miji na namna ya kuziondoa ili kuwa na miji bora na salama kwa vizazi vijavyo.
Imeelezwa katika kongamano hilo kuwa ifikapo mwaka 2050, asilimia 70 ya watu duniani watakuwa wakiishi mijini hivyo kuna umuhimu wa kuwa na mipango madhubuti ya kukabiliana na changamoto za ukuaji wa miji na ongezeko la dadi ya watu.
Tanzania inawakilishwa katika kongamano hilo na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), Wakala wa Barabara za Vijijini ( TARURA) , Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) na Chuo cha Usafirishaji, ambapo miradi mbalimbali na vivutio vilivyopo nchini Tanzania vinaonyeshwa katika Banda la Tanzania, ikiwemo filamu ya The Royal Tour.
MATUKIO MBALI MBALI YA KONGAMANO LA 11 LA MIJI DUNIANI LINALOFANYIKA KATIKA JIJI LA KETOWICE POLAND