![]() |
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa |
RIPOTA PANORAMA
0711 46 49 84
WAZIRI Mkuu, Kassim.Majaliwa jana alitangaza mwelekeo wa Serikali kwa kuainisha mambo itayoyatekeleza na kuyasimamia katika mwaka wa fedha wa 2022/2023.
Akisoma hotuba ya kuhitimisha Bunge la Bajeti, mwaka 2022/ 2023 lililoketi kwa muda wa miezi mitata jijini Dodoma, Waziri Mkuu Majaliwa aliliambia Bunge kuwa miongoni mwa mambo yatakayotekelezwa na kusimamiwa na Serikali ya Awamu ya Sita katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 ni kuendeleza mafanikio yaliyofikiwa sasa katika ukuaji wa Sekta ya Utalii, Nishati, Maji, Miundombinu na uwajibikaji kwenye Serikali za Mitaa.
Waziri Mkuu Majaliwa alisema pamoja na mambo mengine Bunge limepitia, limejadili na kupitisha Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2022/2023.
Alisema Bajeti iliyopitishwa na Bunge imeendelea kuthibitisha nia njema, uthubutu wa hali ya juu na azma ya kweli ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kutelekeza mipango na mikakati mbalimbali yenye lengo la kuwaletea watanzania maendeleo ya haraka sambamba na kuwakwamua kiuchumi.
“Kupitia hotuba hii ya kuhitimisha shughuli za Serikali zilizopangwa kwenye mkutano wa saba wa Bunge la 12, nisingependa kurudia kile kilichokwisha jadiliwa wakati wote wa mkutano huu.
“Hata hivyo, niruhusu nitumie fursa hii kugusia kwa uchache baadhi ya mambo ya msingi ambayo yanaakisi taswira, dhamira, nia, uthubutu, maono na azma ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuhakikisha taifa letu linapiga hatua za haraka za maendeleo ndani ya kipindi kifupi. Miongoni mwa mambo hayo ni ujio wa Filamu ya Royal Tour, ujenzi wa miradi ya maji katika miji 28 na kuwekwa saini kwa makubaliano ya awali ya utekelezaji wa Mradi wa Usindikaji Gesi Asilia (LNG),” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Alisema Filamu ya Royal Tour iliyozinduliwa Aprili 28, 2022 jijini Arusha imeifanya Sekta ya Utalii kuendelea kupata mafanikio makubwa.
Waziri Mkuu Majaliwa alisema filamu hiyo ya kihistoria imekuja kipindi muhimu ambacho Sekta ya Utalii na huduma ilikumbwa na athari za UVIKO-19 lakini baada ya kuzinduliwa imechangia kuimarisha shughuli za utalii na kusaidia kuondoa sintofahamu nyingi kuhusu urithi wa utalii uliopo Tanzania.
“Mheshimiwa Rais ameweza kuonesha uhalisia wa nchi yetu kuanzia vivutio vya biashara, utalii, madini na hata sanaa na utamaduni wetu. Matunda ya jitihada hizo za Mheshimiwa Rais yameanza kuonekana hususan kwenye Sekta ya Utalii na huduma ambapo watalii na wawekezaji kutoka maeneo mbalimbali duniani wameanza kumiminika nchini.
“Mathalan, watu maarufu wakiwemo wachezaji wa mpira wa miguu kutoka ligi kuu mashuhuri barani Ulaya na ligi ya mpira wa kikapu nchini Marekani wametembelea Tanzania katika kipindi hicho. Kadhalika, wakala wa utalii zaidi ya 30 kutoka katika masoko ya utalii yakiwemo ya Marekani, Israeli, Ufaransa na Lithuania wamehamasika kuja nchini ili kujifunza na kujionea vivutio mbalimbali vya utalii kwa lengo la kuvitangaza katika nchi zao,” alisema.
Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa alisema Aprili, 2022 Serikali iliingia makubaliano na Jiji la Dallas lililopo Marekani yenye lengo la kuimarisha ushirikiano katika Sekta za Utalii, Biashara na Uwekezaji, lengo likiwa kufungua fursa za usafiri wa anga kwa safari za moja kwa moja za ndege kutoka Tanzania hadi Jiji la Dallas, Marekani.
![]() |
Ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) |
Alisema lengo la Serikali ni kuendelea kuimarisha miundombinu mbalimbali ya utalii nchini ili kufikia lengo la kuvutia watalii milioni tano kwa mwaka, sambamba na mapato ya Dola za Marekani bilioni sita ifikapo mwaka 2025.
Waziri Mkuu Majaliwa aliliambia Bunge kuwa kuongezeka kwa idadi ya wageni wanaotembelea Tanzania kutaimarisha Sekta ya Utalii na huduma na kutengeneza fursa nyingi zaidi za ajira, kuwakwamua wananchi kiuchumi na kujenga uchumi imara na shindani.
Kuhusu Sekta ya Maji, Waziri Mkuu Majaliwa alisema dhamira ya Rais Samia Suluhu Hasaan imeendelea kujidhihirisha kwenye utekelezaji wa miradi ya maji katika miji 28 uliozinduliwa Juni 6, 2022 yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 500 ambayo itatatua changamoto ya upatikanaji wa maji kwenye miji iliyobainishwa ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Alisema miradi ya maji inayotekelezwa sasa nchini ni mikubwa na itakapokamilika itawezesha upatikanaji wa huduma ya majisafi na usafi wa mazingira kwa wananchi wapatao milioni sita.
Waziri Mkuu Majaliwa alilieleza Bunge kuwa sambamba na upatikanaji wa huduma ya majisafi na usafi wa mazingira, miradi hiyo pia itakuwa chachu ya kuvutia uwekezaji hususan wa viwanda na Serikali itahakikisha ujenzi wa miradi ya maji kwenye miji 28 unafungua fursa nyingine za kiuchumi zikiwemo ajira kwa wananchi kwenye maeneo ambayo miradi hiyo itatekelezwa.
“Nitumie fursa hii kuwasihi Watanzania wenzangu kuchangamkia fursa zitakazojitokeza wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo ili kujiongezea kipato na kujikwamua kiuchumi, niwasihi viongozi na Waheshimiwa Wabunge wenzangu tushirikiane kuimarisha usimamizi wa miradi hii pamoja na kuhakikisha wakandarasi wanakamilisha miradi kwa wakati ili miradi hiyo iweze kutoa huduma iliyotarajiwa kwa wananchi.
![]() |
Rais Samia Suluhu Hassan akiwa katika uzinduzi wa mradi wa maji |
“Vilevile, niwasihi Waheshimiwa Wabunge wenzangu kuwa vinara wa kuhamasisha wananchi kutunza mazingira na kuacha kufanya shughuli za kibinadamu karibu na vyanzo vya maji kwani uhifadhi wa mazingira ndiyo msingi wa uendelevu wa upatikanaji wa majisafi na salama,”alisema.
Hotuba ya Waziri Mkuu Majaliwa alizungumzia pia utekelezaji wa Mradi wa Usindakaji Gesi Asilia (LNG) kwa kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kufanikiwa kutegua kitendawili cha muda mrefu cha utekelezaji wa mradi wa uchakataji LNG uliokuwa umesimama kwa muda mrefu.
Alisema baada ya juhudi kubwa zilizofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita, makubaliano ya awali ya Mkataba wa Nchi Hodhi na Kampuni za Kimataifa za utafutaji Mafuta kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo ulisainiwa Juni 11, 2022.
“Katika kuhakikisha azma ya Mheshimiwa Rais inatimia, nitumie fursa hii kutoa wito kwa viongozi na watendaji wa sekta husika kuhakikisha kuwa utekelezaji wa mradi wa LNG unaleta manufaa yaliyokusudiwa kwa Taifa letu, ikiwa ni pamoja na kuongeza mapato ya Serikali yatokanayo na mauzo ya gesi, kuzalisha ajira za muda mfupi na za kudumu na kuimarisha mapato na uchumi wa Watanzania kupitia mauzo ya bidhaa na huduma mbalimbali wakati wa utekelezaji wa mradi.
“Serikali kwa upande wake itaendelea kuhakikisha inavutia uwekezaji unaokadiriwa kuwa na thamani ya zaidi ya Dola za Marekani bilioni 30 kutoka nje kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo. Vilevile, ninaielekeza Wizara ya Nishati kuhakikisha inatumia vema fursa ya uwepo wa mradi wa LNG kuimarisha uzoefu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC) katika shughuli za gesi pamoja na kuwezesha upatikanaji wa gesi asilia iliyochakatwa kwa ajili ya matumizi ya nyumbani,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
![]() |
Rais Samia Suluhu Hassan akishuhudia utiaji saini makubaliano ya awali ya Mkataba wa NchiHodhi na kampuni za kimataifa za utafutaji mafuta kwa ajili ya Mradi wa Gesi |
Sambamba na yote hayo, Waziri Mkuu Majaliwa alilieleza Bunge kuwa katika mwaka wa fedha 2021/2022, Rais Samia Suluhu Hasaan aliridhia takriban Shilingi bilioni 600 zitumike kwa ajili ya awamu ya pili ya ujenzi wa majengo 25 ya wizara na taasisi kwenye Mji wa Serikali uliopo Mtumba jijini Dodoma.
Alisema ujenzi unaendelea vizuri na kwamba hadi Juni 24, 2022 ulikuwa umefikia kati ya wastani wa asilimia 30 hadi asilimia 56.
“Nitumie nafasi hii kuzihimiza wizara na taasisi kuhakikisha wanaimarisha usimamizi ili ujenzi ukamilike ndani ya muda uliopangwa. Nitoe rai pia kwenu Waheshimiwa Wabunge mnapoondoka hapa bungeni mpate muda kidogo wa kutembelea na kuona kazi nzuri inayoendelea kwenye mji huo,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Hotuba ya Waziri Mkuu Majaliwa alizungumzia pia uwajibikaji katika Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuwa katika kuhakikisha dhamira nzuri ya Rais Samia Suluhu Hassan inayojiakisi kwenye Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2022/2023 inafikiwa, Serikali imejipanga kuendelea kusimamia uwajibikaji katika utumishi wa umma.
Aliitaja mikakati iliyowekwa na Serikali kuimarisha uwajibikaji kwenye Tawala za Mikoa ya Serikali za Mitaa kuwa ni kuongeza bajeti ya matumizi mengineyo katika Ofisi za Wakuu wa Mikoa na Wilaya kutoka Shilingi bilioni 57.44 hadi Shilingi bilioni 79.09 ili kuwezesha utekelezaji wa majukumu ya Ofisi hizo.
Alisema sambamba na ongezeko hilo la Bajeti katika mwaka 2022/2023, Serikali imehuisha muundo wa Sekretarieti za Mikoa kwa kuboresha iliyokuwa sehemu ya usimamizi wa Serikali za Mitaa na kuwa sehemu ya menejimenti, ufuatiliaji na ukaguzi ili kuimarisha ufuatiliaji wa mapato, matumizi na utekelezaji wa miradi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa;
Mkakati mwingine alioutaja ni kuendelea kuwajengea uwezo Mameya, Wenyeviti wa Halmashauri na Miji, Madiwani, Mafisa Tarafa na Watendaji wa Kata kupitia Programu ya Uimarishaji Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuwaongeza uelewa wa majukumu yao kisheria, kuimarisha mahusiano yao na viongozi wa kisiasa na kusimamia ipasavyo miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye maeneo yao pamoja na ukusanyaji wa mapato.
Waziri Mkuu Majaliwa pia alilieleza Bunge kuhusu kuwepo kwa upimaji utendaji wa Wakurugenzi na Wakuu wa Idara kwa kutumia viashiria muhimu hususan usimamizi wa mapato na makusanyo ya ndani, upelekaji wa fedha kwenye miradi ya maendeleo, usimamizi wa mikopo ya asilimia 10 ikiwa ni pamoja na marejesho, usimamizi wa miradi ya maendeleo na uzuiaji na utekelezaji wa hoja za ukaguzi zinazoibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Akiendelea kusoma hotuba yake, Waziri Mkuu Majaliwa alisema kutakuwa na ufuatiiaji na tathimini ambao lengo lake ni kuimarisha utendaji na uwajibikaji serikalini.
![]() |
Bunge la Bajeti 2022/2023 |
“Tasnia hii mtambuka inahitaji uwepo wa mifumo na miundo imara ambayo itawezesha kujenga msingi thabiti wa usimamizi wa utendaji kazi wa Serikali. Kwa kuzingatia hilo, Serikali inaendelea kujenga mifumo na miundo wezeshi katika eneo la ufuatiliaji na tathmini ili kuboresha utendaji kazi unaojali matokeo.
“Hatua hizo zinajumuisha kupitia upya miundo na majukumu ya Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Mashirika ya Umma, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa katika eneo la ufuatiliaji na tathmini ili kuziimarisha pamoja na kujenga uwezo wa watumishi katika eneo hilo,” alisema.
Waziri Mkuu Majaliwa, pia alisema kuwa Serikali imeanza maandalizi ya Sera ya Ufuatiliaji na Tathmini kwa kuzihusisha taasisi simamizi zinazohusika na ufuatiliaji na tathmini ili kuchambua maeneo wanayosimamia na kuhakikisha maeneo yote muhimu yanajumuishwa ikiwemo usimamizi wa mipango ya maendeleo na utendaji wa Serikali kwa ujumla.
Alisema sambamba na hatua hizo, tayari Serikali imekamilisha mfumo wa kitaifa wa usimamizi wa miradi ya maendeleo ambao utaanza kutumika Julai, 2022.
“Mfumo huo, pamoja na mambo mengine utasaidia Serikali kuimarisha ufuatiliaji na tathmini katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na hivyo kuongeza tija na thamani ya matumizi ya fedha za umma kwenye miradi husika. na vilevile, Serikali imehuisha muundo na mgawanyo wa majukumu wa Ofisi ya Waziri Mkuu hususan kwa upande wa Sera, Uratibu na Bunge ili kuimarisha jukumu la ufuatiliaji na tathmini.
“Lengo ni kuhakikisha taarifa za ufuatiliaji na tathmini kutoka katika wizara na taasisi za Serikali zinafanyiwa uchambuzi wa kina pamoja na kutoa mrejesho kuhusu utendaji wa Serikali.
“Ntoe wito kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kushirikiana kwa karibu na Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Fedha na Mipango kufanyia kazi changamoto ya uhaba wa wataalamu wa ufuatiliaji na tathmini; kazi za tathmini kufanyika kwa ufanisi na uwepo wa mifumo mingi ya ukusanyaji wa taarifa yenye kuathiri ubora wa takwimu.
“Serikali itaendelea kufanya tathmini ya ujuzi unaohitajika, kufanya tathmini ya mifumo ya ufuatiliaji na tathmini iliyopo kwenye taasisi za Serikali, kuandaa Kanzi-Data ya watumishi wenye utaalamu wa masuala ya ufuatiliaji na tathmini, kuongeza matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwenye ufuatiliaji na tathmini na kuimarisha vitengo vya ufuatiliaji na tathmini ili kujenga mfumo jumuishi wa ufuatiliaji na tathmini ambao utawezesha kufuatilia, kuchambua na kupata taarifa halisi na kwa wakati za utendaji wa Serikali,” alisema.
Kuhusu ulinzi na uhifadhi wa mazingira, Waziri Mkuu Majaliwa alisema suala la kulinda na kuhifadhi mazingira limeendelea kuwa moja ya vipaumbele muhimu vya Serikali ya Awamu ya Sita.
Alisema mabadiliko ya tabianchi na shughuli za kibinadamu ambazo siyo endelevu na rafiki wa mazingira zikiwemo ukataji wa miti hovyo, uvamizi na uharibifu wa mapori tengefu, ukataji wa miti holela kwa ajili ya uchomaji wa mkaa, uvamizi na uharibifu wa vyanzo vya maji pamoja na uchomaji moto misitu zinachangia uharibifu wa mazingira nchini.
Hotuba ya Waziri Mkuu Majaliwa ilitanguliwa na salamu za pole kwa kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Irene Ndyamukama, pamoja na vifo vilivyosababishwa na ajali za vyombo vya usafiri.
Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa alieleza kuwa Bunge la Baketi lilipata fursa ya kupokea maswali kutoka kwa wabunge na kutolewa majibu kutoka upande wa Serikali, kujadili na kupitisha miswada ya sheria, maazimio ya Bunge na kupokea kauli za Serikali katika kutolea ufafanuzi hoja kadhaa zilizoibuliwa na Wabunge ambazo zilihitaji kupata kauli ya Serikali.
“Latika Mkutano wa Saba wa Bunge la 12, jumla ya maswali 487 ya msingi na mengine 2,622 ya nyongeza yaliulizwa na Waheshimiwa Wabunge na kujibiwa na Serikali. Halikadhalika, jumla ya maswali 27 ya papo kwa papo yaliulizwa na Waheshimiwa Wabunge na kujibiwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu.
“Jumla ya Miswada ya Sheria minne ilijadiliwa na kupitishwa na Bunge. Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali namba mbili wa mwaka 2022 na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji wa mwaka 2022 ilisomwa kwa mara ya kwanza.
“Vilevile, Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2022 na Muswada wa Sheria wa Kuidhinisha Matumizi ya Serikali ilisomwa kwa hatua zake zote,” alisema.
![]() |
Timu ya Serengeti Girls iliyofuzu kucheza mashindano ya Kombe ya Dunia yatakayofanyika India |
Aliyataja maazimio matatu yaliyojadiliwa na kupitishwa na Bunge ambayo jni azimio la Bunge la kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan, baada ya kuwa miongoni mwa viongozi wenye ushawishi mkubwa duniani na kupewa tuzo ya juu ya Mjenzi Mahiri ya Babacar Ndiaye.
Alitaja pia azimio la Bunge la kuipongeza timu ya Taifa ya wanawake ya mpira wa miguu (Serengeti Girls) baada ya kufuzu michuano ya kombe la dunia itakayofanyika nchini India na azimio la Bunge la kuipongeza timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu ya Wenye Ulemavu (Tembo Warriors) iliyofuzu kwenda kwenye michuano ya kombe la dunia itakayofanyika nchini Uturuki.