KISIWA CHA GANA KUPATA KIVUKO KIPYA

Date:

Share post:

 

NA MWANDISHI WETU

CHAMA cha Mapinduzi (CCM), kimeahidi kutoa kivuko kipya kwa wananchi wa kisiwa cha Gana, kilichopo Kata ya Ilangala, wilayani Ukerewe.

Ahadi hiyo imetolewa jana (Ijumaa, Septemba 25, 2020) na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM, Kassim Majaliwa katika mkutano wa kampeni uliofanyika kitongoji cha Gana.

Katika mkutano huo, Majaliwa alimnadi mgombea ubunge wa Jimbo la Ukerewe kupitia tiketi ya CCM, Joseph Mkundi na madiwani. Pia Majaliwa aliwataka wananchi wa Gana wamchague mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Pombe Magufuli katika uchaguzi mkuu ujao wa urais, wabunge na madiwani utakaofanyika Oktoba 28, mwaka huu.

Akitoa ahadi hiyo mbele ya wananchi wa kisiwa cha Gana, Majaliwa alisema uamuzi huo ni utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025 yenye kurasa 303. Kivuko hicho kitatoa huduma kati ya Kakuru na Gana.

Alisema Ilani ya CCM imetoa maelekezo kwa Serikali ijayo itekeleze idadi kubwa ya miradi ya kimkakati ikiwemo kuboresha usafiri wa majini ili kuwandolea adha wananchi wanaoishi katika maeneo ya visiwani.  

Majaliwa alisema wananchi zaidi ya 3000 wa Gana, wanahitaji kivuko bora ambacho kitatoa fursa kwao kufanya shughuli za uvuvi na biashara ili kujipatia kipato.

“Hapa Gana tutaleta kivuko, hiki kisiwa ni kikubwa kina idadi kubwa ya watu ambao wanahitaji huduma bora ya usafiri wa majini. Serikali yenu imeweka mipango mizuri kwa ajili yenu,” alisema Majaliwa.

Alisema chama kitaendelea kutekeleza Ilani yake kwa vitendo kwa kuboresha huduma za wananchi katika visiwa vyote nchini ikiwemo Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza yenye visiwa 38.

Mbali na kutoa ahadi ya kivuko, Majaliwa alisema serikali ijayo itapeleka boti za doria kulinda usalama wa wavuvi ambao wakati mwingine wanafanya shughuli zao kwa mashaka wakihofia uvamizi wa majambazi wanaotoka nchi jirani.

Kwa upande wake, Mkundi alisema kipaumbele cha kwanza baada ya kuingia bungeni ni kuhakikisha serikali ijayo inaboresha huduma ya afya kwa kujenga idadi kubwa ya zahanati ndani ya kisiwa hicho.

“Gana tuna changamoto ya zahanati, umeme na maji. Nitakuwa daraja zuri kati yenu na serikali ili kuhakikisha huduma hizi zinawafikia kwa haraka, naomba mumchague Rais Magufuli ili mambo yetu yaende vizuri,” alisema Mkundi.

Paschal Bukuru ambaye ni mfanyabiashara ya duka, alisema ujio wa kivuko utakuwa mkombozi kwa wananchi wa Gana, kwa kuwa muda mrefu wamekuwa wakitumia mitumbwi kwenda Nansio kufuata mahitaji.

Bukuru alisema wafanyabiashara wamekuwa wakipata changamoto ya kuleta bidhaa zao wakitokea Nansio kwa kuwa hawana usafiri wa uhakika, hivyo ujio wa kivuko hicho utakuwa na manufaa makubwa kwao.

Katika kipindi cha miaka mitano ijayo, CCM imeahidi kuboresha vivuko ikiwemo ujenzi wa kivuko cha Rugezi-Kisorya (Mwanza). Pia ujenzi wa vivuko vipya vinane utaanza ambao ni Ijinga-Kahangala (Mwanza), Musoma-Kinesi (Mara), Nyamisati-Mafia (Pwani), Msangamkuu-Msemo (Mtwara), Nyakalilo-Kome (Mwanza), Bwiro-Bukondo (Ukerewe), Irugwa-Murutanga (Ukerewe) na Kakuru – Ghana (Ukerewe)

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

spot_img

Related articles

JELA MIAKA 30 KWA KUPATIKANA NA BANGI

MAHAKAMA ya Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya imemhukumu Brown Frank Mwaitubi (31), mkazi wa Kajunjumele, kifungo cha miaka...

DUTERTE KUPANDISHWA KIZIMBANI ICC

MANILA, Ufilipino JOPO la majaji watatu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) limethibitisha kuwa Rais wa zamani wa...

WRIGHT: RICE APEWE BALLON D’OR

LONDON, Uingereza MKONGWE wa Arsenal, Ian Wright, amemtaja Declan Rice kuwa anastahili kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka...

ISRAEL, LEBANON ZAONGEZA WIKI TATU ZA KUSITISHA VITA

WASHINGTON DC, Marekani RAIS wa Marekani, Donald Trump, amesema Israel na Lebanon zimekubaliana kuongeza wiki tatu za kusitisha mapigano. Wakati...