MALABO, Guinea ya Ikweta
KIONGOZI wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Leo XIV, ameeleza kutokuridhishwa na namna wafungwa wanavyoishi katika magereza nchini Guinea ya Ikweta.
Papa ameyasema hayo alipotembelea magereza ya nchi hiyo, ambapo aliyakuta kwenye hali mbaya.
Gereza maarufu la Bata alilotembelea Kiongozi huyo wa Vatican limekuwa likinyooshewa vidole na wanaharakati wa haki za binadamu.
Kwa mujibu wa Shirika la Haki za Binadamu la Amnesty International, Gereza hilo ni ‘jehanamu’ ya wakosoaji wa Serikali.
Baadhi ya wafungwa wamenyimwa haki ya kukutana na ndugu zao na hawajulikani kama wako gerezani, kwa mujibu wa Amnesty International.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Waziri wa Sheria wa Guinea ya Ikweta, Reginaldo Biyogo Ndong, si kweli kwamba wafungwa wamekuwa wakiteswa katika gereza hilo.
Akizungumza na wafungwa, Papa Leo amewaambia: “Hamko peke yenu. Familia zenu zinawapenda na zinawasubiri. Watu wengi nje ya kuta za gereza wanawaombea.”






