Sunday, June 22, 2025
spot_img

MAJALIWA: TAKWIMU ZA SENSA NI MUHIMU KWA WAFANYABIASHARA, SERIKALI

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa


RIPOTA WA WAZIRI MKUU

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema takwimu za Sensa ya Watu na Makazi zitawasaidia wafanyabiashara kutathmini uwezo wao wa kibiashara au uwezo wa mitaji kutoa faida na kutafuta maeneo mapya ya uwekezaji.

 

Hayo ameyasema jana katika ukumbi wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na wadau wa sekta binafsi juu ya umuhimu wa ushiriki wao kwenye Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika Agosti 23, 2022.

 

Alisema wafanyabishara wakubwa na wadogo hutumia takwimu za sensa kutathmini uwezo wa kibiashara wa makampuni, uwezo wa mitaji kutoa faida na kutafuta maeneo mapya ya uwekezaji na kupitia takwimu za sensa, menejimenti na bodi za makampuni ya biashara na taasisi za uwekezaji za ndani na nje hupata uhakika wa kitakwimu ambao huwaongezea kujiamini na kufanya maamuzi sahihi na kwa wakati. 

 

Waziri Mkuu Majaliwa alisema wafanyabiashara wakubwa kwa wadogo wanategemea takwimu za sensa kufanya maamuzi ya uwekezaji ikiwemo huduma mbalimbali kama maduka makubwa, upanuzi wa shughuli zao kama maghala ya kuhifadhia na kusambazia bidhaa, maeneo bora ya kutangaza biashara zao, masoko mapya na kubuni bidhaa mpya pamoja na aina ya huduma kama za hospitali, sehemu za starehe na sehemu za kufanyia mazoezi.

 

Aidha, alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuridhia, kuthamini na kutilia mkazo mkubwa masuala ya takwimu na kuruhusu mwaka huu Tanzania ifanye Sensa kwa mujibu wa miongozo ya Umoja wa Mataifa.

 

“Kitendo cha Mheshimiwa Rais kuridhia kutekeleza sensa ya sita mwaka huu kinaonesha uimara wa uongozi wa kiongozi wetu na utekelezaji wa takwa hili ni kwa faida ya nchi yetu na ulimwengu kwa jumla.

 

“Sensa ya watu na makazi ni muhimu kwa kuwa moja ya mikakati ya kiuchumi ya Tanzania ni kuvutia uwekezaji na kuboresha kiwango cha maisha cha wananchi wake. Uwepo wa takwimu bora za sensa ya watu na makazi utasaidia kuharakisha utekelezaji wa mikakati hiyo,” alisema.

 

Akizungumzia umuhimu wa sensa kwa wafanyabiashara, alisema kwa jumuiya ya wafanyabiashara, sensa ni chanzo cha msingi cha taarifa za kidemografia na ukuaji wa soko la bidhaa na huduma katika nchi zote duniani na kwamba takwimu zote za biashara zinahitaji takwimu za idadi ya watu kama kigezo cha msingi cha kufanya maamuzi ya uwekezaji, uzalishaji na biashara.

 

Waziri Mkuu Majaliwa alivipongeza vyombo vya habari kushiriki kutoa hamasa na kuieleza jamii jamii umuhimu wa sensa na kwamba utafiti uliofanywa na Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) Julai, mwaka huu ulionesha kuwa asilimia 98 ya Watanzania wanatambua uwepo wa sensa

 

“Kitendo cha kuwaonesha wananchi nini kitaulizwa, kimesaidia kuwaandaa wananchi kuhusu zoezi hili. Wasanii mbalimbali nchini wametoa elimu kwa kiwango kikubwa, viongozi wa dini nao wamefanya kazi kubwa na nzuri sana ya kuwaandaa wananchi, ninawashukuru sana,” alisema.

 

Akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na wadau hao, Waziri wa Nchi, Ofisi ya  Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, George Simbachawene alisema mpaka sasa maandalizi ya sensa yamefikia asilimia 95.

 

“Asilimia hii tano iliyobakia tusiidharau. Kulingana na muda uliobaki, mimi pamoja na wenzangu tutajitahidi ili tufike kwenye ufanisi unaotarajiwa wa asilimia 100,” alisema.

 

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Paul Makanza alisema wameshirikiana na Serikali katika vikao kadhaa na kuainisha maeneo saba ambayo wanaweza kuunga mkono.

 

Aliyataja baadhi ya maeneo hayo kuwa ni utoaji wa huduma, vifaa, utoaji elimu, usafiri, usafirishaji wa vifaa, utoaji wa matangazo na kuchangia mafuta ya magari. Alisema baadhi ya kampuni za simu zilianza kurusha jumbe fupifupi kwa wateja wao, vituo vya redio na televisheni nazo zilirusha matangazo kuhamasisha jamii.

 


Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya