TEHRAN, Iran
MOJA ya habari zilizotikisa vichwa vya habari duniani kwa siku za hivi karibuni ni wakati mgumu anaopitia mwanaharakati wa haki za binadamu nchini Iran, Narges Mohammadi.
Narges anayesota gerezani, ameripotiwa kukabiliwa na hali mbaya ya kiafya wakati huu akiendelea kusota gerezani.
Taarifa iliyotolewa na mwanasheria wake, ilidai kuwa mshindi huyo wa tuzo ya Amani ya Nobel ya Mwaka 2023 alikimbizwa hospitali baada ya afya yake kutetereka.
“Alipata maumivu makali ya kifua, kisha afya yake ikazorota zaidi,” alisema mwanasheria wake, Mostafa Nili, na kusisitiza kuwa huduma za matibabu anazopewa mteja wake haziendani na hali yake.
Familia yake ikaeleza pia, kwamba afya ya Narges mwenye umri wa miaka 54 haijaimarika tangu alipopata shambulio la moyo mwishoni mwa Machi, 2026.
KWANINI ANASOTA GEREZANI?
Kilichomponza ni harakati zake za kupambania haki za wanawake, pamoja na kuipinga Serikali, ikiwamo msimamo wake wa kutokukubaliana na adhabu ya kifo nchini Iran.
Kutokana na ukosoaji wake kwa Serikali, Narges amekuwa akiingia na kutoka katika kuta za gereza kwa miaka mingi, tangu alipokamatwa kwa mara ya kwanza mwaka 1998.
Hata hivyo, wakosoaji wa Serikali wanasema mashitaka dhidi yake yanatokana na kazi nzuri anayoifanya ya utetezi wa haki za binadamu.
Safari hii, alikamatwa baada ya kutangaza kifo cha mwanaharakati mwenzake wa haki za binadamu, Khosrow Alikordi, ambaye alitajwa kuuawa na mamlaka.
Waendesha mashitaka wa Iran walidai kuwa Narges alieneza ujumbe wa chuki katika hotuba yake siku ya maziko ya Alikordi, alipowataka wahudhuriaji kutokukaa kimya katika changamoto zinazowakabili.
Alikamatwa Desemba, 2025 na kuhumiwa kifungo cha miaka 10 gerezani, kabla ya kuongezwa miaka saba na nusu ya kuendelea kuishi kwenye kuta za gereza.
Baada ya hukumu, alihamishwa kutoka Tehran na kupelekwa Zanjan, ambako hana ndugu na hali ya gereza ni mbaya zaidi.
FAMILIA YALAANI, YATAKA AACHIWE
Katika taarifa yao, familia ya Narges imelaani kitendo cha mamlaka za gereza kuchelewa kumpeleka hospitali mwanaharakati huyo, ikidai hatua hiyo ilikuja baada ya madaktari wa gerezani kuona tatizo limekuwa kubwa.
Katika hatua nyingine, familia imetaka Narges kuachiwa, ikisema mashitaka dhidi yake ni matokeo ya Serikali kuchukizwa na ukosowaji wake.






