BAADA ya sare ya mabao 2-2 jana Mei 3, 2026, mechi inayozikutanisha Simba na Yanga, maarufu kwa jina la ‘Kariakoo Derby’, imeandika historia mpya Ligi Kuu Bara.
Simba ikiwa mwenyeji wa mchezo huo uliochezwa katika Uwanja wa Jenerali Isamhuyo jijini Dar es Salaam, ilifunga mabao yake kupitia kwa Libasse Gueye na Clatous Chama, huku Yanga ikisawazisha kupitia kwa Prince Dube na Bakari Nondo Mwamnyeto.
Rekodi zinaonesha kuwa ni mara ya kwanza baada ya miaka mitatu kwa ‘derby’ ya Kariakoo kushuhudia mabao manne yakifungwa ndani ya dakika 90 za Ligi Kuu Bara.
Mara ya mwisho kuona idadi hiyo ikipatikana ilikuwa Novemba 5, 2023, ambapo Simba ikiwa mwenyeji wa mchezo ilikubali kichapo cha mabao 5-1.
Mabao ya Yanga katika derby hiyo yalifungwa na Kennedy Musonda, Maxi Nzengeli (mawili), Stephanie Aziz Ki na Pacome Zouzoua, huku Kibu Denis akipachika kwa upande wa Simba.
Kwa upande mwingine, mara ya mwisho kwa Simba na Yanga kumaliza dakika 90 za Ligi Kuu zikiwa na matokeo ya sare ya mabao 2-2 ilikuwa Januari 4, 2020.






