Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Amos Gabriel Makalla amesema ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa uwanja wa michezo wa mashindano ya Africa Cup of Nations pamoja na barabara za kuingia katika uwanja huo, huku akisisitiza kasi iongezwe ili miradi hiyo ikamilike kwa wakati na kwa ubora uliokusudiwa.
Mhe. Makalla ametoa kauli hiyo leo Jumanne Mei 05, 2026 wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya miradi hiyo inayotekelezwa katika Kata ya Olmot, jijini Arusha ambapo Amesema uwanja huo unatarajiwa kukamilika ifikapo Agosti 2026, huku ujenzi wa barabara za kuingia uwanjani ukitarajiwa kukamilika Mei 2027, miezi michache kabla ya kuanza kwa mashindano ya AFCON 2027.
“Nimefurahi na maendeleo haya na tuna uhakika kwamba kabla ya Michuano ya AFCON mwakani mwezi Agosti, tutakuwa tayari tumeshakamilisha uwanja huu kwa mwaka mmoja kabla. Aidha, barabara za kuingia uwanjani zitakuwa zimekamilika ifikapo Mei 2027, miezi mitatu kabla ya mashindano,” amesema Makalla.
Aidha Ameongeza kuwa serikali ipo tayari kwa mashindano hayo makubwa barani Afrika na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha upatikanaji wa fedha za miradi hiyo kwa wakati, hatua inayowezesha ujenzi kwenda bila changamoto za kifedha.
“Wakandarasi hawana shida ya fedha, malipo yanafanyika kwa wakati kulingana na mkataba. Hii ni ishara kwamba Tanzania tupo tayari kwa AFCON,” amesisitiza makalla.
Kwa upande wao, wasimamizi wa mradi kutoka kampuni ya China Railway Construction Engineering Group wameeleza kuridhishwa na ushirikiano wa serikali na kusema miradi hiyo inatarajiwa kukamilika kwa ubora wa hali ya juu na kwa muda uliopangwa huku wakiahidi kuendelea kuongeza kasi ya ujenzi ili kuhakikisha Tanzania inakuwa tayari kwa mashindano hayo makubwa ya mpira wa miguu barani Afrika.






