Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, amesema Wizara yake itaendelea kuimarisha udhibiti wa upotevu wa maji katika mifumo ya usambazaji kwa kutumia teknolojia za kisasa katika mwaka wa fedha 2026/2027.
Akiwasilisha bajeti ya Wizara ya Maji, Aweso ameeleza kuwa hatua hiyo itahusisha matumizi ya mifumo ya usomaji mita kwa njia ya kielektroniki, ufuatiliaji wa mtandao wa maji (smart water management system), ukarabati wa miundombinu chakavu pamoja na ufungaji wa dira za maji za malipo kabla.
Alisema lengo la hatua hizo ni kuongeza ufanisi katika usambazaji wa maji na kupunguza upotevu unaotokana na hitilafu za kiufundi pamoja na matumizi yasiyo halali.
Aidha, Waziri Aweso amebainisha kuwa Wizara itaendelea kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya watu wanaojihusisha na uharibifu wa miundombinu ya maji na wizi wa maji, vitendo ambavyo vinachangia kwa kiasi kikubwa upotevu wa rasilimali hiyo muhimu.
Vilevile, amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kujenga uwezo wa wataalam wa sekta ya maji ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia za kisasa, hatua itakayosaidia kuhakikisha usanifu wa miradi ya maji unakuwa imara na vifaa vinavyotumika vinakidhi viwango vinavyotakiwa kulingana na mahitaji ya miradi husika.






