LONDON, Uingereza
MICHELLE na Lavinia Osbourne walipishana dakika chache tu kuzaliwa kwao. Ni mapacha waliotokana na mama mmoja lakini baba tofauti.
Si ajabu. Kitaalamu, hiyo inawezekana kupitia mchakato adimu wa kibaolojia unaofahamika kwa jina la ‘heteropaternal superfecundation’.
Ni endapo mwanamke anapozalisha mayai mawili au zaidi wakati wa mzunguko mmoja, kisha yakarutubishwa na wanaume wawili tofauti.
Hata hivyo, kama ilivyoelezwa awali, ni adimu hilo kutokea. Ni mara 20 pekee yameripotiwa matukio ya aina hiyo duniani kote.
Kuthibitisha hilo, Lavinia na Michelle ndiyo mapacha pekee wa baba tofauti kuwahi kutokea katika ardhi ya Uingereza.
Michelle na Lavinia walizaliwa mwaka 1976 mjini Nottingham, wakati huo mama yao akiwa na umri wa miaka 19 tu.
Wakiwa na umri wa miaka mitano, mama yao aliwaacha na kwenda kusoma London, hivyo akawaacha kwa rafiki yake pale Nottingham.
Baada ya mama yao kufariki Februari 14, 2022, Michelle alishawishika kuanza kufuatilia aliko baba yao, ingawa tayari walishatajiwa jina la James.
Wiki chache baadaye, Michelle alibaini kuwa James hakuwa baba yao. Na badala yake, aligundua kwamba mzee wake ni Alex, kaka wa rafiki wa mama yao.
Si tu vipimo vya DNA kuthibitisha, bali pia aliamua kujiridhisha kwa kuwatafuta ndugu wa Alex, na ndipo alipobaini kuwa anafanana nao kwa kiasi kikubwa.
Kazi ikabaki kwa Lavinia. Naye aliamua kufanya uchunguzi, akihusisha pia vipimo vya DNA kama alivyofanya pacha wake, Michelle.
Akabaini kuwa baba yake ni Arthur. Lavinia na Michelle walifunga safari hadi Magharibi mwa London kumfuata na kufanya naye mazungumzo, ambapo Arthur alikiri kuwa ndiye baba mzazi wa binti huyo.






