Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeanza kutumia uzoefu wa bandari kubwa duniani katika kuboresha na kuendeleza miundombinu yake, hatua inayolenga kuongeza ufanisi wa huduma, kuvutia uwekezaji na kuimarisha ushindani wa Tanzania katika biashara ya kimataifa.
Hatua hiyo inakuja wakati TPA ikijiandaa kuanza kutekeleza Tozo ya Maendeleo ya Miundombinu ya Bandari (Ports Infrastructure Development Levy), mfumo maalumu wa kufadhili upanuzi wa miundombinu ya bandari na kuongeza uwezo wa kuhudumia mizigo inayoongezeka kutokana na ukuaji wa biashara ndani na nje ya nchi.
Kwa mujibu wa taarifa za TPA, tozo hiyo itaanza kutumika Julai 1, 2026 kwa kiwango cha asilimia 4.5 ya thamani ya CIF ya shehena, baada ya kiwango kilichopendekezwa awali cha asilimia 9 kupunguzwa kufuatia mashauriano na wadau mbalimbali wa sekta ya biashara na usafirishaji.
Mapato yatakayopatikana kupitia tozo hiyo yanatarajiwa kusaidia ujenzi na ukarabati wa magati, kuongeza uwezo wa kupokea na kuhifadhi mizigo, kuboresha huduma za usafirishaji na kuweka msingi wa miundombinu itakayokidhi mahitaji ya biashara ya miaka ijayo.
Katika utekelezaji wa mkakati huo, TPA imeeleza kuwa inajifunza kutoka kwa baadhi ya bandari zinazoongoza duniani zikiwemo Port of Rotterdam, Port of Singapore, Port of Shanghai, Port of Hong Kong, Port of Los Angeles, Port of Hamburg, Port of Antwerp, Jebel Ali Port pamoja na Tanger Med.
Bandari hizo zimekuwa zikihudumia mamilioni ya makontena na mamia ya mamilioni ya tani za mizigo kila mwaka, huku zikiunganisha masoko ya mabara mbalimbali kupitia usafirishaji wa mafuta, gesi, magari, bidhaa za viwandani, mazao ya kilimo na bidhaa za matumizi ya kila siku.
Inaelezwa kuwa kwa miaka mingi bandari hizo zimekuwa zikitumia tozo na ada mbalimbali za watumiaji kama chanzo muhimu cha kugharamia maendeleo ya miundombinu yake, jambo lililowezesha kuongeza uwezo wa kuhudumia mizigo, kuvutia biashara zaidi na kuimarisha mchango wake katika uchumi wa dunia.
Wachambuzi wa sekta ya usafirishaji wa baharini wanasema ushindani wa bandari za kisasa haujengwi kwa kuangalia mahitaji ya sasa pekee, bali kwa kuwekeza katika miundombinu inayoweza kukidhi mahitaji ya biashara ya miaka 10, 20 na hata 30 ijayo, hatua ambayo inaweza kuifanya Tanzania kuwa kitovu muhimu cha biashara na usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.







