Mwaka 2018, Serikali ilianza utekelezaji wa kuboresha Tanzania Ports Authority kupitia Bandari ya Tanga kwa lengo la kuifanya kuwa kitovu muhimu cha biashara na usafirishaji si kwa Tanzania pekee, bali kwa ukanda mzima wa Afrika Mashariki na Kati.
Baada ya maboresho hayo makubwa, Bandari ya Tanga imebadilika kutoka bandari ya zamani iliyokuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali hadi kuwa lango muhimu la biashara linalopokea meli kubwa kutoka sehemu mbalimbali duniani zikiwa zimebeba mizigo kwa ajili ya Tanzania na nchi jirani.
Bandari hiyo sasa imejijengea sifa ya kuwa salama kwa mizigo, yenye huduma bora kwa wateja na mazingira yanayoakisi ukarimu wa watu wa pwani ya Afrika Mashariki.
Lakini zaidi ya hayo, Bandari ya Tanga ni sehemu yenye historia kubwa. Ni miongoni mwa bandari kongwe katika ukanda wa Afrika Mashariki, ikianza kutoa huduma tangu miaka ya 1880 wakati wa utawala wa wakoloni wa Kijerumani walioipa jina la “Marine Jet.”
Wakati huo hakukuwa na magati ya kisasa kama ilivyo leo. Kulikuwepo sehemu maalumu ya mwinuko iliyotumika kupakia na kupakua mizigo kutoka kwenye vyombo vya usafiri wa majini.
Historia inaonyesha kuwa maboresho ya kwanza ya bandari hiyo yalifanyika mwaka 1914 kwa kujengwa kwa gati la kwanza, kabla ya kuongeza gati jingine mwaka 1954.
Hata hivyo, kadri miaka ilivyopita na teknolojia ya usafiri wa majini kuendelea kubadilika, miundombinu hiyo ilianza kupitwa na wakati. Magati yaliyokuwepo hayakuwa tena na uwezo wa kuhudumia meli kubwa za kisasa kutokana na changamoto mbalimbali za miundombinu na ufanisi wa huduma.
Kutokana na hali hiyo, mwaka 2018 Serikali kupitia Tanzania Ports Authority ilianza rasmi utekelezaji wa maboresho makubwa ya Bandari ya Tanga.

Leo, kauli imegeuka kuwa uhalisia.
Meneja wa Bandari ya Tanga, Salehe Mbega, katika mahojiano maalumu na Tanzania Panorama amesema Serikali kupitia Tanzania Ports Authority imewekeza zaidi ya Sh. bilioni 429.1 katika maboresho ya bandari hiyo kati ya mwaka 2019 na 2022.
Anasema maboresho hayo yalihusisha ujenzi wa magati mapya, uchimbaji wa kina cha bandari pamoja na ununuzi wa mitambo ya kisasa ya kuhudumia mizigo.
“Maboresho haya yameibadilisha kabisa Bandari ya Tanga. Ujenzi wa gati moja pekee unaweza kugharimu kati ya Sh. bilioni 250 hadi 300 ukijumuisha vifaa na mitambo,” anasema Mbega.
Kwa mujibu wa Mbega, maboresho yaliyofanyika mwaka 1914 na 1954 yalikuwa na manufaa makubwa kwa wakati huo, lakini hayakuweza tena kuendana na mahitaji ya sasa ya usafirishaji wa kisasa wa majini.

Anasema hatua ya Serikali kuwekeza katika maboresho hayo imeiwezesha Bandari ya Tanga kuingia katika ushindani wa kimataifa.
Mkuu wa Idara ya Utekelezaji katika bandari hiyo, Gwakisa Mwaibuji, anasema moja ya mafanikio makubwa yaliyopatikana ni kupungua kwa gharama za uendeshaji.
Anaeleza kuwa kabla ya maboresho, shughuli nyingi za kupakia na kupakua mizigo zilifanyika nangani, hali iliyosababisha matumizi makubwa ya muda na fedha kutokana na mfumo wa “double handling.”
“Kabla ya maboresho tulikuwa tunafuata mizigo kwenye meli kubwa zilizokuwa mbali na gati, tunaipakia kwenye vyombo vidogo kisha kuileta bandarini. Mfumo huo ulikuwa ghali na wenye usumbufu mkubwa,” anasema.
Anasema hivi sasa meli kubwa zinaingia moja kwa moja bandarini na kuhudumiwa kwa urahisi, jambo lililopunguza gharama na kuongeza ufanisi wa huduma.
Mwaibuji anaongeza kuwa maboresho hayo yameifanya Bandari ya Tanga kuwa kivutio kikubwa kwa meli za mizigo mbalimbali, ikiwemo zinazobeba bidhaa za ammonium na sulphur ambazo hapo awali hazikuwa zikitumia bandari hiyo.
“Kwa sasa tunapokea wastani wa meli kubwa 20 kila mwezi. Mwitikio wa wateja umeongezeka sana,” anasema.
Mbega naye anasema ongezeko la shughuli za bandari limechangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa mapato ya Serikali kupitia Tanzania Revenue Authority.
Aidha, anasema Bandari ya Tanga sasa inahudumia nchi nyingi zaidi za ukanda huu zikiwemo Democratic Republic of the Congo, Zambia, Malawi, Rwanda, Burundi, Uganda, Kenya na Zimbabwe.
“Bandari sasa inafanya kazi mchana na usiku. Mizigo imeongezeka kwa kiwango kikubwa sana,” anasema.
Kutokana na ongezeko hilo la mizigo, Tanzania Ports Authority ilianzisha yadi ya Mwambani kwa ajili ya kuhifadhi mizigo mbalimbali.
Mbega anasema yadi hiyo yenye ukubwa wa takribani hekari 174 imewekewa uzio, taa, umeme pamoja na mifumo ya kisasa ya ulinzi.
Anasema eneo hilo lina uwezo wa kuhifadhi magari hadi 1,500 kwa wakati mmoja, mengi yakiwa yanaelekea katika nchi jirani.
“Yadi hii imetusaidia kuongeza uwezo wa kuhifadhi mizigo na kupokea shehena nyingi zaidi bila usumbufu,” anasema.
Katika upande wa sekta binafsi, wadau mbalimbali wa biashara wameeleza kufurahishwa na maboresho hayo.
Meneja wa Kampuni ya Uwakala wa Meli ya Seafront Shipping, Amri Sufian, anasema maboresho ya Bandari ya Tanga yameongeza kwa kiasi kikubwa shughuli za kampuni yao.
“Hapo zamani bandari haikuwa na uwezo wa kupokea meli kubwa, lakini sasa sisi kama Seafront Shipping tunaingiza wastani wa meli nane kwa mwezi,” anasema.
Anaongeza kuwa katika kipindi cha miaka miwili baada ya maboresho, kampuni hiyo imefanikiwa kuingiza zaidi ya meli kubwa 70 bandarini hapo.
Tozo za Mizigo na Vivutio kwa Wateja
Bandari ya Tanga pia imeweka mfumo rafiki wa tozo za mizigo ili kuvutia wafanyabiashara wengi zaidi.
Kwa mujibu wa Meneja wa Bandari hiyo, mizigo mingi huanza kutozwa baada ya siku 15 tangu kuhifadhiwa bandarini, tofauti na baadhi ya bandari nyingine ambapo tozo huanza ndani ya siku tano hadi saba.
Kwa mizigo ya Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo, muda wa kutotozwa umeongezwa hadi siku 30 kufuatia makubaliano maalumu yaliyofikiwa ili kuvutia matumizi makubwa ya Bandari ya Tanga.
Fursa za Ajira na Nafasi ya Wanawake

Mbali na kuongeza biashara, maboresho ya Bandari ya Tanga pia yamefungua milango ya ajira kwa wananchi wengi wa Tanga na maeneo jirani.
Mwenyekiti wa Wafanyakazi wa Kutwa bandarini hapo, Ayubu Kinyama, anasema zamani ilikuwa vigumu kupata kazi bandarini kutokana na uhaba wa shughuli.
“Mtu alikuwa anaweza kukaa siku nzima bandarini bila kupata kazi. Lakini sasa watu wengi wanapata ajira kila siku na wengine wameanzisha biashara zao kutokana na shughuli za bandari,” anasema.
Katika hatua nyingine, wanawake nao wameendelea kunufaika na fursa zilizotokana na maboresho hayo.
Farida Dhahabu, ambaye ni dereva wa forklift na winch bandarini hapo, anasema zamani kazi hizo zilionekana kuwa za wanaume pekee.
“Mwanzoni tuliamini kazi hizi ni za wanaume, lakini sasa wanawake wanapata nafasi kubwa na wanafanya vizuri. Tunaishukuru Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutupa fursa hizi,” anasema Farida.

Maboresho ya Bandari ya Tanga yameiweka bandari hiyo katika nafasi nzuri ya ushindani wa kimataifa huku ikiendelea kuwa mhimili muhimu wa biashara kwa Tanzania na nchi jirani.
Kutoka “Marine Jet” ya miaka ya 1880 hadi kuwa kitovu kikubwa cha biashara katika ukanda wa kaskazini, Bandari ya Tanga sasa ni alama ya mafanikio ya uwekezaji wa kimkakati wa Serikali katika sekta ya usafirishaji wa majini.








