Serikali ya Marekani kupitia Wizara yake ya Mambo ya Nje imetangaza kumuwekea vikwazo Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi Tanzania, Mafwele kwa kupigwa marufuku kuingia nchini humo kutokana na tuhuma za kuhusika katika ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.

Taarifa hiyo iliyotolewa Mei 21, 2026 na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, imeeleza kuwa hatua hiyo imechukuliwa chini ya Kifungu cha 7031(c) cha sheria ya Marekani, kinachoruhusu kuwekwa kwa vikwazo dhidi ya maafisa wa serikali za kigeni wanaotajwa kuhusika moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja katika vitendo vya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mwaka 2025 maafisa wa Jeshi la Polisi Tanzania walidaiwa kuwakamata, kuwatesa na kuwafanyia ukatili wa kingono raia wa Uganda, Agather Atuhaire, pamoja na raia wa Kenya, Boniface Mwangi, walipokuwa jijini Dar es Salaam kufuatilia mwenendo wa kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu.

Marekani imesema kutokana na taarifa hizo na ushahidi uliopatikana, imeamua kumuwekea Mafwele vikwazo vya kutoruhusiwa kuingia nchini humo. Aidha, uamuzi huo umetangazwa hadharani kwa mujibu wa sheria ya National Security, Department of State and Related Programs Appropriations Act ya mwaka 2026.

Hadi sasa, Jeshi la Polisi Tanzania pamoja na Serikali bado hawajatoa tamko rasmi kuhusiana na hatua hiyo iliyotangazwa na Marekani.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here