Serikali kupitia wizara ya viwanda na Biashara imesema mauzo ya bidhaa za Tanzania katika soko la kimataifa yameongezeka kwa asilimia 16 mwaka 2025, hatua inayotajwa kuchochewa na kuimarika kwa mazingira ya biashara pamoja na upanuzi wa masoko ya bidhaa za ndani.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga amesema thamani ya biashara ya Tanzania nje ya nchi imefikia dola za Marekani milioni 10,080.9 mwaka 2025 kutoka dola milioni 8,702 mwaka 2024.

Akizungumza bungeni jijini Dodoma leo Mei 22, 2026 wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Kapinga amesema ongezeko hilo limetokana na uzalishaji mkubwa wa bidhaa zinazokidhi ushindani wa soko la kimataifa pamoja na kupatikana kwa masoko mapya.

Amesema mazao ya kilimo yaliyoongoza kuuzwa nje ya nchi ni ufuta, tumbaku, mbaazi, ngano, mchele, maharage, mahindi, kahawa, pamba na parachichi.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, bidhaa nyingine zilizochangia kuongezeka kwa mauzo nje ya nchi ni samaki, dhahabu, kakao, makaa ya mawe, vigae na mabati.

Katika kuendelea kukuza sekta ya viwanda na biashara, wizara imeomba Bunge kuidhinisha zaidi ya Shilingi bilioni 137.8 kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Ambapo fedha hizo zitaelekezwa katika kuimarisha sekta ya viwanda, biashara na uwekezaji ili kuongeza uzalishaji wa ndani na ajira kwa Watanzania katika mwaka 2025/2026 huku viwanda vipya 25 vya kati na vikubwa vimeanzishwa nchini na kutoa zaidi ya ajira 39,000.

Sambamba na hayo Waziri kapinga amesema Tanzania kwa sasa ina viwanda 1,604 vya kuzalisha mafuta ya kula, huku viwanda vikubwa vikiwa 14, vya kati tisa, vidogo 543 na vidogo sana 1,038 ambapo viwanda hivyo vina uwezo wa kuzalisha tani 2,527,739 za mafuta kwa mwaka na vimetoa ajira za moja kwa moja 10,755 pamoja na ajira zisizo za moja kwa moja 36,416.

Hata hivyo, ameongeza kuwa uzalishaji wa mafuta ya kula bado haujakidhi mahitaji ya ndani kutokana na viwanda vya ndani kuzalisha tani 302,000 pekee kati ya mahitaji ya zaidi ya tani 700,000 kwa mwaka Kutokana na hali hiyo amesema tani 430,000 za mafuta ya kula huagizwa kutoka nje ya nchi ili kuziba pengo la mahitaji ya soko la ndani.

Sanjari na hayo Kapinga amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuongeza uzalishaji wa mafuta ya kula nchini ikiwemo utoaji wa mbegu bora, ruzuku ya mbolea, kuhamasisha uwekezaji katika mbegu za mafuta na kuboresha teknolojia kwa wasindikaji wadogo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here