MKAZI WA GEITA MBARONI KWA KUFUKIA MTOTO WAKE AKIWA HAI

Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita linamshikilia Amina Shabani (21), mkazi wa Kijiji na Kata ya Muungano, Wilaya ya Chato, kwa tuhuma za kumfukia mtoto wake mchanga wa jinsia ya kike akiwa hai ndani ya shimo muda mfupi baada ya kujifungua.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safía Jongo amesema tukio hilo limetokea Mei 16, 2026 majira ya alasiri baada ya kujifungua mapema siku hiyo majira ya saa nne asubuhi.

Tukio hilo lilibainika Mei 17, 2026 baada ya wananchi kusikia sauti ya mtoto mchanga ikitokea nyuma ya nyumba ya mtuhumiwa bila kuonekana mtoto huyo na ndipo wakatoa taarifa Jeshi la Polisi ambalo lilifika eneo la tukio na kumuokoa mtoto huyo.

Mtoto huyo alikimbizwa katika Hospitali ya Wilaya ya Chato kwa matibabu na uchunguzi wa kitabibu, ambapo baadae alifariki dunia Mei 18, 2026 akiwa anapatiwa huduma.

Baada ya tukio hilo, mtuhumiwa alikimbia na kujificha kwa lengo la kukwepa mkono wa sheria, lakini Jeshi la Polisi lilimfuatilia na kumkamata akiwa katika harakati za kutoroka kwenda mkoa jirani.

Chanzo cha tukio hilo bado kinachunguzwa, na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here