MAAFISA MAENDELEO YA JAMII ARUSHA WAKUTANA KUTATHIMINI MALEZI NA ULINZI WA WATOTO

MAAFISA wa maendeleo ya jamii na ustawi kutoka Halmashauri ya Jiji la Arusha, Arusha DC na Wilaya ya Meru wamekutana leo Mei 20, 2026 kufanya tathmini ya utekelezaji wa muongozo wa vikundi vya malezi, huku wakisisitiza umuhimu wa kuendelea kuunda vikundi hivyo katika kata mbalimbali ili kuimarisha malezi na ulinzi wa watoto kwenye jamii.

Akizungumza katika kikao hicho, Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Arusha, Helena Materu amesema kikao hicho kimewakutanisha wadau mbalimbali kujadili mafanikio, changamoto na mbinu za kuboresha uundaji na usimamizi wa vikundi vya malezi kuelekea maadhimisho ya Siku ya Familia Duniani na Siku ya Mtoto wa Afrika mwezi Juni.

Amesema kupitia kikao kazi hicho pia wamebadilishana uzoefu kuhusu namna ya kuendesha vikundi hivyo kwa ufanisi, huku akizitaka kata ambazo bado hazijaanzisha vikundi vya malezi kufanya hivyo haraka ili kuongeza ushiriki wa jamii katika malezi ya watoto.

“Tumekutana pia na Maafisa Kilimo, Mifugo, Lishe pamoja na Maafisa Ustawi wa Jamii kujadiliana namna ya kupambana na ukatili katika jamii,” amesema Bi. Materu.
Kwa upande wake, Mratibu wa Malezi Mbadala, Ulinzi na Usalama wa Mtoto kutoka Shirika la SOS Children’s Villages, Husna Selungwi amesema Mkoa wa Arusha una vikundi 31 vya malezi vyenye walezi 816, ambapo zaidi ya 700 ni wanawake.

Bi. Selungwi ametoa hamasa kwa wanaume kuendelea kujiunga katika vikundi hivyo akieleza kuwa vinasaidia kuimarisha malezi bora na ustawi wa watoto katika jamii.
Naye Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Elibarick Neiman amesema ameridhishwa na mwitikio wa wanaume kuhamasishwa kushiriki kwenye vikundi hivyo vya malezi.

Aidha, Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Arusha DC, Beatrice Tengi amesisitiza umuhimu wa kuanzishwa kwa vituo vya kulelea watoto mchana (Community Day Care), huku akiwataka wananchi kufika katika ofisi za ustawi wa jamii kupata taratibu za kuanzisha vituo hivyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here