
Serikali imeendelea kuboresha elimu kwa kuwapatia mafunzo walimu wapya 266 wa masomo ya Sayansi na Hisabati kwa lengo la kuimarisha ufundishaji na kuinua ufaulu katika masomo hayo kwa ajili ya maendeleo ya taifa.
Akifungua mafunzo ya siku tano Mei 20,2026 kwa walimu hao kutoka mikoa ya Iringa na Dodoma, Afisa Elimu Taaluma Mkoa wa Dodoma, Sophia Mbeyu, amesema mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za serikali katika kuboresha ufundishaji wa masomo ya Sayansi na Hisabati nchini.
Amesema mafunzo hayo yanafanyika kwenye Shule ya Sekondari ya Dodoma kupitia Mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari nchini (SEQUIP), unaosimamiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais–TAMISEMI.
“Walimu wanapatiwa ujuzi wa kutumia mbinu mpya za ufundishaji zinazolenga kuongeza uelewa wa wanafunzi na kupandisha kiwango cha ufaulu kwa masomo hayo,”amesema Sophia.
Ameeleza kuwa miongoni mwa mbinu zinazofundishwa na wawezeshaji ni matumizi ya darasa janja, ambalo linatumia teknolojia kuwaunganisha walimu kutoka maeneo mbalimbali ili kujifunza kwa pamoja na kubadilishana uzoefu wa ufundishaji.
Aidha, walimu hao wanafundishwa matumizi ya teknolojia katika ufundishaji pamoja na utengenezaji wa zana za kufundishia kwa kutumia vifaa vinavyopatikana katika mazingira yao, ili kurahisisha uelewa wa wanafunzi.
Amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwasaidia wanafunzi kuelewa kwa kina masomo ya Sayansi na Hisabati na kuyapenda, hususan kutokana na changamoto ya baadhi yao kuyakwepa.
“Walimu wa Sayansi na Hisabati tumieni mbinu mtakazopata hapa kuwafundisha watoto wetu. Hakikisheni mnawaandaa vizuri ili kila shule iwe na idadi kubwa ya wanafunzi wanaosoma masomo ya Sayansi,” amesema Sophia.
Kwa upande wake, Afisa Elimu Mwandamizi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Oscar Msalila, amesema serikali inaendelea kuwekeza katika mafunzo ya walimu kupitia SEQUIP ili kuwajengea uwezo wa kutumia mbinu za kisasa za ufundishaji.
Amesema lengo la mafunzo hayo ni kuinua kiwango cha elimu nchini, hususan katika masomo ya Sayansi na Hisabati ambayo ni msingi muhimu katika kuzalisha wataalamu wa sayansi na teknolojia watakaosaidia maendeleo ya taifa.







