WANANCHI CHUNYA WALALAMIKIA KUCHUKULIWA FEDHA KWA AHADI YA UMEME

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa, ameliagiza Jeshi la Polisi mkoani humo, kumtafuta mtu anayedaiwa kujihusisha na utapeli wa fedha kwa wananchi wa Wilaya ya Chunya kwa ahadi ya kuwaunganishia huduma ya umeme, ili arejeshe fedha hizo pamoja na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Hatua hiyo imekuja kufuatia malalamiko ya baadhi ya wakazi wa kijiji cha Mtakuja, kata ya Nkung’ungu Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya, waliodai kuchukuliwa Shilingi 35,000 kila mmoja kwa ahadi ya kuunganishiwa umeme bila huduma hiyo kutolewa.

Wananchi hao wameeleza kuwa mtu huyo alikuwa akijitambulisha kama afisa kutoka TANESCO na kuwaahidi kupata huduma ya umeme kwa haraka, jambo lililowafanya wengi kutoa fedha kwa matumaini ya kuunganishiwa umeme majumbani mwao.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi walioathirika wameiomba Serikali pamoja na vyombo vya usalama kuchukua hatua kali dhidi ya vitendo vya udanganyifu vinavyoendelea kuwaumiza wananchi, hususan maeneo ya vijijini.

Kwa upande wake, Msamimazi wa Miradi wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA) Wilaya ya Chunya, Hamis Said, amesema mtu anayehusishwa na tuhuma hizo si mfanyakazi wa TANESCO wala REA, akieleza kuwa anadaiwa kuwa na ujuzi wa masuala ya umeme pamoja na leseni kutoka EWURA.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here